SHEIN KUHUTUBIA BUNGE LA EAC KESHO
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein leo anatazamiwa kulihutubia Bunge la Afrika ya Mashariki ambapo jumla ya miswada mitatu itawasilishwa.
Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Daniel Kidega alisema hayo wakati akizungumza na waandishi habari katika ofisi ya Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya mji wa Unguja.
Alisema maandalizi ya kikao hicho yamekamilika ikiwemo wabunge wote wa nchi za EAC wapo Zanzibar ambapo kikao hicho kinafanyika baada ya kipindi cha miaka kumi.
Aliitaja miswada itakayowasilishwa katika bunge hilo ni pamoja na muswada wa kuleta usawa wa kijinsia katika taasisi za kutunga sheria ambao utawasilishwa na Mbunge kutoka Kenya, Nany Abisia.
Abisia alisema, kwa mfano Kenya hadi sasa haijazingatia usawa wa kijinsia katika taasisi hadi bunge la nchi hiyo lenye wajumbe 400, huku wanawake wanaotoka katika majimbo ya uchaguzi ni 10 tu.
“Idadi ya wanawake katika chombo cha kutunga sheria hairidhishi hata kidogo zaidi kwa upande wa Kenya ambapo idadi ya wanawake katika vyombo vya uamuzi ni ndogo sana,” alisema.
Aidha, Kidega alisema muswada wa kulinda mazingira na kupunguza uharibifu wa matumizi ya vifaa vya plastiki utawasilishwa mbele ya bunge hilo.
Waziri wa zamani wa mazingira nchini Rwanda, Patricia Hjabakiga alisema kumejitokeza tatizo la uharibifu wa mazingira kwa vifaa vya plastiki katika nchi za jumuiya hiyo na kusababisha athari kubwa za kimazingira.
Katika kikao cha wiki mbili cha Bunge la Afrika ya Mashariki pia taarifa mbalimbali za kamati za bunge zitawasilishwa mbele ya wajumbe kwa ajili ya kujadiliwa.
Disqus Comments