MISRI YASHUTUMIWA KUCHOCHEA MACHAFUKO ETHIOPIA
Ethiopia imeituhumu serikali ya Misri kuwa ndiyo inayochochea machafuko nchini humo.
Getachew Reda, Waziri wa Habari na Msemaji wa Serikali ya Ethiopia amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa kwamba machafuko yaliyotokea wiki iliyopita katika eneo la Oromo, la magharibi mwa nchi hiyo, yalichochewa na maadui wa nje hususan Misri ambao alidai, lengo lao ni kuvuruga utulivu wa Ethiopia.
Msemaji wa Serikali ya Ethiopia ameituhumu Misri kuwa inaipa fedha na mafunzo ya kijeshi harakati ya Ukombozi wa Oromo ambayo inapigania kujitenga eneo hilo na Ethiopia. Amedai kuwa, kundi hilo linapata uungaji mkono wa pande zote kutoka kwa serikali ya Misri.
Amesema, serikali ya Ethiopia inaihesabu harakati ya Ukombozi wa Oromo kuwa ni kundi la kigaidi na kudai kuwa, huko nyuma viongozi wa kundi hilo walikuwa wakiishi mjini Asmara, Eritrea na hivi sasa wamehamia Cairo, mji mkuu wa Misri.
Vile vile amesisitiza kuwa, baadhi ya wanasiasa wa Misri wanafurahi kuona hali ya utulivu inatoweka nchini Ethiopia na wanafanya hivyo baada ya kukasirishwa na hatua ya Ethiopia ya kujenga bwawa la al Nahdha kwa lengo la kufaidika zaidi na maji ya Mto Nile ambao Misri inauhesabu kuwa ni mshipa wake wa uhai.
Disqus Comments