Kijana aumwa tena na buibui uumeni Australia
Mwanamume wa umri wa miaka 21 nchini Australia ameumwa tena na buibui mwenye sumu kali uumeni.
Alikuwa anaenda haja katika eneo ambalo ujenzi umekuwa ukiendelea Jumanne mjini Sydney alipoumwa karibu pahala sawa na alipoumwa miezi mitano iliyopita.
Jordan, ambaye hakutana kufichua jina lake la ukoo, alisema aliumwa karibu eneo sawa na aliloumwa awali.
"Nafikiri mimi ndiye mtu mwenye mkosi zaidi nchini kwa sasa," aliambia BBC.
"Nilikuwa nimeketi chooni nikiendelea na shughuli zangu nilipohisi uchungu wa ghafla kama niliouhisi wakati ule. Sikuamini kwamba limefanyika tena. Niliangalia chini na nikaona miguu kadha imechomoza."
Amesema tangu alipoumwa mara ya kwanza, amekuwa akihofia sana kutumia vyoo vya muda.
"Baada ya kisa hicho cha kwanza, kusema kweli sikutaka kuvitumia tena," anasema.
"Vyoo huoshwa siku hiyo na nilifikiria ilikuwa wakati mwafaka kwangu kuvitumia. Niliangalia vyema chini kabla ya kuketi kuanza shughuli yangu. Kushtukia, mimi huyo naumwa tena."
Mwenzake alimkimbiza hospitali ya Blacktown.
Alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani lakini kuna uwezekano kwamba huenda asitumie vyoo vya muda tena.
Mtu anapoumwa na buibui hupata maumivu makali, kutokwa na jasho na pia kupata kichefuchefu.
Ingawa kumewahi kuripotiwa visa vya watu kufariki baada ya kuumwa na buibui aina ya redback, hakuna aliyefariki tangu kugunduliwa kwa dawa ya kumaliza sumu mwaka 1956.
Disqus Comments