Kenya yampata jaji mkuu mpya, David Maraga
Jaji David Maraga ameapishwa kuwa Jaji Mkuu mpya wa Kenya baada ya kustaafu kwa jaji mkuu wa awali Dkt Willy Mutunga.
Jaji Maraga atakuwa jaji wa pili kuhudumu nchini Kenya tangu kuanza kutekelezwa kwa katiba ya sasa nchini Kenya, ambayo ilifanyia mabadiliko mfumo wa mahakama, mwaka 2010.
Ameapishwa baada ya kuidhinishwa na bunge siku ya Jumanne.
Moja ya shughuli muhimu anazotarajiwa kutekeleza ni kuwaapisha wanachama wa jopo la kuteua makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Kenya inapoendelea kujiandaa kwa uchaguzi mkuu Agosti mwaka ujao.
Kama jaji mkuu, atakuwa pia Rais wa Mahakama ya Juu ambayo husikiliza na kutoa uamuzi kuhusu kesi za matokeo ya uchaguzi wa urais.
Wakati wa kuhojiwa kwake na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), kabla ya jina lake kupendekezwa kwa rais, alikuwa amedokeza kwamba hawezi kufanya kazi siku ya Jumamosi ambayo ni siku ya kupumzika kwa mujibu wa dini yake ya Kiadventisti.
Hata hivyo, ameonekana kusisitiza umuhimu wa kutumiwa kwa njia mbadala za kutatua mizozo katika jamii.
Disqus Comments