Abiria wa Ndege walazimishwa kupima uzani
Shirika moja la ndege Marekani limelalamikiwa na wateja wake kwa kuwalazimisha kupima uzani kabla ya kuingia ndani ya ndege zao. Lalama hizo zimetolewa na wafanyibiashara wawili kutoka Kisiwa cha American Samoa.
Wawili hao wameambia Mamlaka ya uchukuzi nchini Marekani kwamba walilazimishwa kupima uzani wao wakati wakianza safari yao kutoka mji wa Honolulu. Kituo cha Radio nchini New Zealand kimesema raia hao walikerwa sana waliponyimwa haki ya kuchagua viti vyao kwenye ndege kutokana na uzani wao. Walikua wakitoka Kisiwani Hawaii kuelekea mji wa Pago Pago.
Masharti ya abiria kupima uzani yamewekewa raia wa Kisiwa cha America Samoa, baada ya Kisiwa hicho kutajwa kuongoza kuwa na watu wanene kupindukia duniani.
Raia wa kisiwa hicho kilichoko Bahari ya Pacific wameripotiwa kupenda vyakula vyenye mafuta mengi na hawafuati lishe bora. Mtu mmoja kati ya watu watatu anaugua kisukari katika Kisiwa cha American Samoa. Kwa sasa mamlaka ya uchukuzi Marekani imesema inachunguza lalama za wafanyibiashara hao.
Disqus Comments