Home
ELIMU YA AFYA MAGONJWA NA TIBA
UTAFITI: Kiwango cha Elimu ya Mama ni kigezo cha Uwezo wa mtoto katika kufaulu au kufeli shuleni
UTAFITI: Kiwango cha Elimu ya Mama ni kigezo cha Uwezo wa mtoto katika kufaulu au kufeli shuleni
Utafiti wa ripoti ya tano iliyofanywa na taasisi ya Twaweza kuhusu uwezo wa watoto nchini wanaosoma shule za serikali, umebaini licha ya kuwepo kwa mipango mikakati isiyokidhi haja ya ubora wa elimu nchini kutoka serikalini, lakini kiwango cha elimu ya mama wa mtoto kimebainika kuwa kigezo cha kusababisha kiwango cha ufaulu wa mtoto shueni.
Wazazi wenye elimu kuanzia sekondari na kuendelea, wanaonekana kuwa na watoto wanaofanya vizuri masomoni wawapo shuleni katika mazoezi, majaribio na mitihani yao wanayoifanya.
Ripoti hiyo iliyopachikwa jina “Je watoto wetu wanajifunza? Hali ya Elimu ya Tanzania mwaka 2015 na kuendelea” iliyofanyika mwaka 2014 (jumla ya watoto 32,694 walipimwa kutoka kaya 16,013. Takwimu pia zilikusanywa kutoka shule za msingi 1,309) inaonesha kuwa, Kwa wastani, mama mwenye kiwango kikubwa cha elimu, watoto wake wanakuwa na matokeo mazuri kwenye majaribio ya Uwezo ya kusoma ugha ya kiingereza, kiswahili na kufanya hesabu kuhesabu.
Watoto wa darasa la tatu 3 hadi darasa la 7 katika shule za misingi za serikali zilizofanyiwa utafiti, ufaulu wao katika majaribio ya masomo unaonesha kuwa juu kwa watoto wenye wazazi waliosoma kiwango kuanzia sekomdari zaidi ya wale ambao elimu za mama zao ni kuanzia elimu ya msingi na kushuka chini.
Asilimia ya wanafunzi wa darasa la 3-7 waliofaulu majaribio ya Kiswahili, Kingereza na Hisabati kutokana na kiwango cha elimu cha mama.
– Watoto 8 kati ya 10 (81%) ambao mama zao wana elimu ya sekondari walifaulu jaribio la Kiswahili kulinganisha na watoto 6 kati ya 10 (63%) ambao mama zao hawajapata elimu yoyote rasmi.
– Watoto 5 kati ya 10 (54%) ambao mama zao wana elimu ya sekondari walifaulu jaribio la Kingereza ukilinganisha na watoto 2 tu kati ya 10 (22%) ambao mama zao hawakuwa na elimu yoyote rasmi.
– Watoto 7 kati ya 10 (69%) ambao mama zao wana elimu ya sekondari walifaulu jaribio la hesabu ukilinganisha na wanafunzi 4 tu kati ya 10 (44%) ambao mama zao hawakuwa na elimu yoyote rasmi.
Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Peramiho, iliyoko mkoa wa Ruvuma wilaya ya Songea Vjijini, Mwl. Jane Ndomba, wakati wa uzinduzi wa utafiti huu, alitoa mchango wake katika kipengele hiki, ambapo alisema wazazi waliosoma hasa wanawake wanakuwa chachu katika kufatilia maendeleo ya watoto wao wakiwa shueni na hata wakiwa tayari wamerudi nyumbani kwa kuwafatilia na kuwasaidia katika kufanya mazoezi waiopewa na walimu wao shuleni.
Pia alibainisha mwamko wa mwanamke anayekuwa na elimu jinsi anavyozidi kuithamini elimu ya mwanae kwa kuwa na hamu ya mtoto wake kufuata nyayo zake, hivyo huwa mstari wa mbele hata katika kuitikia mikakati inayopangwa na shule husika katika kuendeleza ufaulu wa wanafunzi shuleni, kama vile kuchangia chakula shuleni, kuwawezesha walimu wasio na makazi.
Vile vile, utafiti huu unaonesha sababu nyingine zinazohusu ubovu wa utendaji kazi wa serikali, unaochangia ufaulu wa wanafunzi kuwa duni, baadhi ya mambo yaliyogundulika ni kama ifuatavyo.
Watoto wengi wanaanza elimu ya msingi bila kupitia masomo ya elimu ya awali (Chekechea), hali hii inapelekea watoto kuanza masomo ya darasa la kwanza wakiwa wageni wa kila kitu na hatimaye kuleta matokeo mabaya ya kutokujua kusoma wala kuandika hai inayoendelea hadi kumaliza darasa la saba, kwani wanakosa msingi mzuri tangu mwanzoni.
Kuhusu masomo ya chekechekea, mpango wa sera ya serikali unasema, kila shule ya msingi inapaswa iwe na darasa la awali pamoja na mwalimu au walimu wa kufundisha, lakini suala hili halitekelezwi katika shule zote, na hali hii inaonekana kupuuziwa kwani ufatiliaji na utatuzi wa jambo hili haupo kwa kiwango kinachohitajika huku wanafunzi wa vijijini wakiwa wahanga wa kiwango cha juu zaidi ya wale wanaishi mijini.
Utafiti huu unaonesha kuwa moja kati ya shule tano za msingi za serikali, asilimia 20% zilizofanyiwa utafiti, hazikuwa na madarasa wala elimu ya awali , pia watoto 6 kati ya 10 (64.7%) wenye umri wa kwenda shule za awali miaka 5-6, hawajaandikishwa kuanza, huku asilimia 35.3% pekee ndio walioandikishwa kupata elimu ya awali.
Disqus Comments