Kamari za mpira, unyonyaji mpya uangamizao vijana
SERA ya Ujamaa na Kujitegemea iliyoasisiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1967 ililenga kuthamini utu, kuleta umoja na mshikamano Tanzania.
Leo hii ukizungumzia sera hii ya Ujamaa watu watashangaa na kuona umepitwa na wakati.
Japokuwa Katiba yetu (ya mwaka 1977) inaeleza Tanzania ni nchi ya Kijamaa na misingi ya Ujamaa inaainishwa vizuri, lakini sivyo ilivyo kiuhalisia kwani, Tanzania sasa imeshakuwa nchi ya kibepari inayoongozwa na mabepari wa nchi za Magharibi na mabepari uchwara wa ndani ya nchi.
Baada ya Tanzania na nchi nyingine za Kiafrika kukaribisha soko huria (Free market) thamani ya utu ikaisha na bidhaa zikapata thamani zaidi kuliko binadamu (Co-modification). Hii ndio sifa kubwa ya ubepari (Capitalism) ambayo hupuuza thamani ya utu na kuipa nguvu kubwa bidhaa.
Leo hii, tunashuhudia Tanzania ikiwa na mabepari uchwara (Petty bourgeoisies) walioweka utu nyuma na kujali maslahi yao binafsi kwa kuzidi kuwanyonya maskini walio wengi. Hichi ndicho kilichokuwa kinapingwa na sera ya Ujamaa ambayo ilitaka usawa na kuthamini utu wa Mtanzania.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kitabu chake kiitwacho ‘Reflection on Leadership in Africa’ anasema: “Na hakutakuwa na watu wa kizazi hiki na karne hii ambao watatakiwa kujitoa muhanga kwa ajili ya maisha bora katika siku zijazo wakakubali, wakati wanawaona watu wachache wakiendelea kuneemeka machoni pao bila kujali wakati ujao, wakati wao (wananchi) na watoto wao wakiendelea kuishi maisha duni na dhalili”.
Mabepari uchwara hawa wamejaa Tanzania wakitambulika kwa majina mbali mbali kama vile ‘wajasiriamali’, ‘wawekezaji wa ndani’ na hata pia ‘wafanyabiashara’. Mabepari uchwara hawa wanafanya yale yote ambayo ubepari unataka kwa kuzidi kuwanyonya Watanzania wenzao kwa maslahi yao binafsi na kusahau jamii yao kwa ujumla. Ndio maana leo utashuhudia huduma nyingi za kijamii kama vile elimu na afya zikiuzwa kwa wingi na mabepari uchwara hawa kwa gharama kubwa.
Hebu sasa, tuangalie hawa mabepari uchwara wanaowanyonya vijana wetu kwa kiasi kikubwa kwa kupitia kamari za mipira.
Yamkini, wengi wetu tumeshasikia ama kushiriki katika kamari hizi za mipira (football betting). Leo hii ukizunguka miji mingi Tanzania biashara hii ya kucheza kamari kwa ligi mbali mbali za mpira ya nchi za magharibi imeshamiri sana.
Kamari hii imeshamiri katika kubashiri matokeo ya mpiria ya ligi za Uingereza, Hispania na Ujerumani. Tujiulize kwanini si ligi za mpira za ndani ya nchi yetu? Mathalani mechi dhidi ya Lipuli na Mbeya City? Au Morogoro United dhidi ya Prisons.
Kamari hii ya kubashiri matokeo ya mpira ya ligi za nchi za Magharibi imekuwa ni jinamizi lililowakumba vijana wengi wa Kitanzania.
Kila ukipita katika kona za miji ya Tanzania hususan karibu na kumbi za kuonyesha mipira utakuta vijana walivyolundikana wakigombania tiketi kwa ajili ya kubashiri matokeo. Tiketi hizi hulipwa kwa gharama tofauti tofauti kulingana na ubashiri huo utakavyokuwa mgumu ama mwepesi.
Tanzania inakoelekea sasa itakuwa na taifa la vijana wasiopenda kufanya kazi bali kupata pesa kwa njia rahisi kama hizi za kubashiri matokeo ya mpira. Kamari sasa imehalalishwa licha ya sote kutambua kwamba ni haramu. Ndiyo maana hapo awali ilikuwa ikiruhusiwa kwenye klabu maalum tu, siyo mitaani kama ilivyo sasa.
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, ubepari haujali utu wa mtu hata kidogo na ndicho wanachokifanya hawa mabepari uchwara waliowekeza kwenye kamari za mpira. Vijana wengi walio na kazi na wasio na kazi, wasomi na wasio wasomi wote mawazo yao sasa yako kwenye kupata pesa kirahisi bila ya kutumia jasho wakisahau yule anayepata faida kati yao wabashiri matokeo na mabepari uchwara hao.
Inasikitisha kuona vijana wengi wa vyuo vikuu leo ukipita katika vyuo vyao na kuwaona wanavyogombania tiketi za kubashiri matokeo ya mpira. Mara nyingi najiuliza, inakuwaje wasomi hawa tunaowategemea wanashindwa kuona unyonyaji huu na kuzidi kuukimbilia? Sasa kama wasomi hawa ndicho wanachokifanya ni nani atakuja kulikomboa taifa letu dhidi ya udhalimu huu?
Hebu tuangalie namna ambavyo kamari hii ya mpira ni janga kwa vijana wa Kitanzania.
Kwanza kabisa, vijana hutumia muda mchache kuzalisha mali kwani muda mwingi hutumia kuangalia mpira ili kuweza kuyasadiki matokeo ya mpira na kuona kama wameshinda au la. Na ukiangalia kwa undani utagundua ni asilimia ndogo sana ya vijana wanaobashiri hushinda wengi wao huishia kuliwa pesa zao tu bila mafanikio yoyote.
Hivi karibuni kupitia televisheni ya BBC-Dira ya Dunia, tumeshuhudia kijana wa Kitanzania aliyekuwa akicheza kamari za mpira huko nchini Kenya alipoamua kumchoma mwezake kisu baada ya kuliwa takribani Dola 300 (shilingi za Kitanzania 630,000).
Hii inatuonyesha fika kabisa unyonyaji huu unawatia vijana wetu matatani kwa kujiingiza katika vurugu zisizo na msingi. Hapa bepari uchwara huyu ameshapata fedha zake na kuacha vijana wakiangamia, kwani anachojali hapa ni fedha na siyo utu.
Kwa kuwa kamari inalevya (addiction) kama vile utumiapo vilevi vya sigara ama pombe, inampasa kijana kufanya kila mbinu kupata pesa kwa ajili ya kwenda kubashiri matokeo.
Leo hii utaona wimbi la vibaka wadogo wadogo likizidi kuongezeka ili wapate fedha, utapeli unazidi kila kukicha ili kuwapatia watu fedha, utoro katika shule za bweni unaongezeka na ongezeko la wanafunzi kufeli kila mwaka kutokana na kutumia muda wao mwingi katika vibanda vya mipira kubashiri matokeo.
Mabepari uchwara hawa hawataki kujua madhara wanayoyaleta kwa jamii ila kile wanachojali wao ni fedha kwani kamari hii ya mpira inawapatia fedha nyingi sana bila ya kutumia nguvu zozote zile.
Mabepari uchwara hawa hutumia ujuha wetu kutajirika, wao hukaa na kusubiri tuwapelekee fedha zetu kirahisi tu. Vijana wengi sasa wanazidi kuangamia katika janga hili kila kukicha na bado hatuoni kama ni tatizo. Au kwa kuwa nchi inapigia debe ‘wawekezaji wa ndani’ hatupaswi kuangalia maswahibu yanayowakumba vijana wetu?
Ni wakati sasa serikali ikaliangalia hili kwa jicho la karibu kabisa kwani likiendelea kwa miaka kadhaa ijayo tutakuwa na taifa tegemezi kupita kiasi.
Je, kamari katika mpira ina tofauti gani na wakati ule watu walivyokuwa wakiweka pesa zao ‘DECI’ ambako watu walikuwa wakipanda mbegu (pesa) na kuvuna mavuno makubwa kirahisi tu. Ndipo tuliposhtuka na kuona tunaibiwa na seirkali kuamua kupiga marufuku biashara hiyo ya pesa. Na je sasa tunasubiri mpaka vijana wetu waangamie kabisa ndipo tupige marufuku kamari hii ya mpira wa miguu?
Au inatofauti gani na michezo mingine ya kamari ambayo imepata kuwapo na kuwaacha wananchi wakiwa maskini zaidi huku wachache kupata utajiri wa ghafla kupita kiasi. Ni kama enzi za “jackpot bingo” ikawaacha wananchi wakisubiri bingo.
Kila siku tunajiuliza namna ya kumkomboa kijana katika wimbi la umaskini na tumekuwa tukipiga debe wajifunze ujasiriamali ili kujikomboa na umaskini. Sasa vijana hawa watatokaje kwenye umaskini huu kama kile wapatacho ndicho hukipeleka kwa mabepari uchwara hawa wa kubashiri matokeo ya mpira?
Kama nia ya kumsaidia kijana wa Kitanzania kuondokana na umaskini hatuna budi kuangalia suala hili upya.
Sera ya Ujamaa na Kujitegemea ilionekana mbaya na kuanza kupingwa na wengi hatimaye ikatupiliwa mbali, lakini aina hii ya wizi, unyonyaji na udhalimu haukuwepo wakati huo.
Kama vijana wa zamani walitunzwa kwenye mazingira ya haki na utu, iweje leo tunawaachia vijana wetu kutumbikia katika janga hili kwa kuhalalisha biashara sisizo na tija kwa jamii zaidi ya kuongeza unyonyaji kwa vijana maskini wa kitanzania?
Wakati umefika sasa, aina hii ya unyonyaji uliohalalishwa unapaswa kupigwa vita vikali sana ili kuweza kuwanusuru vijana wetu katika dhuluma hii.
Serikali, familia na jamii yote kwa ujumla inatupasa kuamka sasa na kuanza kukemea na kusitisha unyonyaji huu ambao unazidi kuharibu vijana wetu.
Ni jukumu letu sote sasa, kama jamaa moja kulikomboa taifa letu na hasa vijana wetu waliotumbukia kwenye dimbwi hili la kamari ya mpira.
Disqus Comments