Tyson Fury: WBO kutwaa mkanda wa ubingwa wa dunia
Bingwa wa uzani wa juu wa ndondi duniani, Mwingereza Tyson Fury amepewa siku 10 na WBO kueleza ni kwa nini hafai kupokonywa mkanda wake wa ubingwa.
Alijiondoa kutoka kwa pigano la marudiano na Wladimir Klitschko wa Ukraine mapema mwezi huu kwa sababu ya matatizo ya kiakili.
Bondia huyo wa miaka 28 pia anakabiliwa na mashtaka ya kutumia dawa zisizoruhusiwa.
Kwenye mahojiano na runinga moja wiki iliyopita, alikiri kutumia kokeini kukabiliana na msongo wa mawazo.
Mwenyekiti wa WBO Luis Batista-Salas amesema Fury huenda akapoteza mkanda huo kwa "kutoshiriki mapigano, kuvunja mkataba na kwa kutumia dawa zilizoharamishwa."
Hata hivyo amesema WBO wanajali sana hali yake ya kiafya na wanamtakia afueni ya haraka.
Fury ndiye pia bingwa wa WBA.
Fury hajapigana tangu amshinde Klitschko Novemba mwaka jana.
Disqus Comments