NYUMBA YA MAAJABU [31-36]
NYUMBA YA MAAJABU: 31
Sophia na Ibra waliondoka eneo lile huku wakiwa na mawazo hata kumsahau Siwema ambaye walienda nae pale, walirudi nyumbani kwao moja kwa moja na kuingia ndani, walikaa sebleni wakiwa wamejawa na mawazo wakasikia sauti ya mtu akicheka kugeuka wakamuona Neema akicheka.
Tena alicheka zaidi baada ya wao kumuona vizuri, walishtuka sana na kujikuta wakisema kwa pamoja,
“Neema!!!!”
“Ndio ni mimi au mnahisi mmenifananisha?”
Ibra alimuangalia Sophia ambaye hakujiweza kwa muda ule na kuanguka pale kwenye kiti.
“Jamani Neema unataka kuniulia mke wangu?”
“Kumuua siwezi, hata usiwe na shaka”
“Sasa umefanya nini?”
Neema akacheka tena na kusema,
“Nimfanye nini huyo na uoga alionao? Huwa sishughuliki na watu waoga, humu ndani rafiki yangu ni wewe ila hujijui tu. Mimi ndio Neema, siku zote nawaambia kuwa ni ngumu sana kuniondoa mimi humu labda niamue mwenyewe kuondoka. Ila ninachotaka kukwambia ni kuwa msitoke hapa nyumbani kwako kwa muda wa siku tatu yani msiende popote halafu baada ya siku hizo mimi ndio nitapotea kabisa humu ndani”
“Kwani wewe Neema ni mtu wa aina gani?”
“Hata ukijua haitakusaidia zaidi zaidi itakuzidishia uoga tu, ni bora usijue chochote.”
“Ila mimi nina kinga zangu”
Neema akacheka tena na kumwambia Ibra,
“Kinga? Kinga ni kitu gani? Sijaamua tu Ibra sababu bado nakuhitaji sana tu, kama huamini uliza kwa makini kilichompata huyo mganga wenu. Mimi ndio Neema mwingine sio mimi. Ila weka akilini hakuna kutoka nje hadi siku tatu zipite”
Kisha Neema akaondoka pale na kumuacha Ibra akiwa anashangaa shangaa tu, ila leo hakuwa na uoga kama ambao alikuwa nao siku zote kisha akambeba mke wangu na kwenda nae chumbani.
Baada ya muda mfupi Sophia nae akazinduka huku akijishika kichwa na kujiuliza kuwa ni nini kimetokea,
“Kwahiyo hukumbuki kabisa Sophia?”
“Sikumbuki chochote”
“Ngoja nikukumbushe”
Ibra alianza kumwambia Sophia hatua kwa hatua juu ya matukio ya siku hiyo, kwakweli Sophia alibaki kushangaa tu,
“Kheeee kwahiyo huyo neema kasema tusitoke hapa?”
“Ndio alivyosema mke wangu yani hadi namshangaa”
“Sasa tutajuaje kinachoendelea kuhusu huyo mganga uliyeniambia?”
“Kujuaje mke wangu wakati mganga mwenyewe ameshakufa!”
“Mmh basi mume wangu naomba tumtii huyo Neema huenda atafurahi na kuondoka kweli”
“Sophia huwa unachukulia kirahisi rahisi sana ila kiukweli huyu Neema si mtu mzuri hata tukisema tumtii ni kazi bure”
“Sasa unafikiri tufanyaje?”
“Ngoja nitakwambia tu cha kufanya”
Sophia akatulia kimya huku muda huo Ibra nae akatulia kimya halafu muda kidogo akainuka na kuelekea chooni, ila gafla alirudi huku akiwa anahema sana
“Vipi tena mume wangu?”
“Kheee kuna maajabu chooni”
“Maajabu gani tena?”
Ibra hakuweza kuelezea ila alionekana akitetemeka tu, muda kidogo simu yake ikaanza kuita na kuipokea. Aliyekuwa akipiga alikuwa ni Siwema
“Hivi nyie mmeenda wapi? Mbona mmekimbia?”
“Hatujakimbia ila tulipatwa na mshtuko na kuondoka”
“Hivi mnajua kuwa nyie ndio chanzo cha kifo cha huyu mzee?”
“Chanzo kivipi jamani?”
“Kwahiyo hamjijui eeeh!!”
“Hatujui chochote”
“Kama hamjui kwanini mmeondoka gafla? Sasa huku wametoa siku moja tu muwe mmekuja bila ya hivyo nimeambiwa kitakachowapata sijui”
Kisha Siwema akakata ile simu na kumfanya Ibra amuangalie mkewe ambaye alihitaji kujua haswaa kile ambacho kilikuwa kikiongelewa na Siwema, Ibra akapumua kidogo na kuanza kumsimulia mke wake.
“Jamani yani sisi ndio tumesababisha kivipi?”
“Hata mimi mwenyewe nashangaa”
“Sasa tutafanyaje wakati hata hapa tumekatazwa kutoka hadi siku tatu zipite?”
Ibra akajikuna kichwa bila ya kuwa na jibu la aina yoyote ile, akafikiria kitu kidogo na kusema
“Nadhani huu ni mtego”
“Mtego!! Kivipi?”
“Sijui kivipi ila nahisi kamavile Neema anatufanyia mchezo, haiwezekani atukataze kutoka kwa siku tatu halafu huko tupewe siku moja tuwe tumeenda. Yani huu ni mtego kabisa Sophia”
“Hebu tuangalie la muhimu ni lipi, kwenda huko au kukaa ndani kwa siku tatu na Neema apotee?”
Wakajifikiria na kukosa jibu kabisa kisha wakaamua kulala tu kwa muda huo.
Wakati wamelala Sophia akajikuta akiyaona matukio karibia yote kwenye ndoto, kwanza kabisa alimuona yule mganga alipofika pale kwao na yote aliyoyafanya hadi kuondoka, Badae akamuona yule mganga akiwa nyumbani kwake kisha akamuona akielekea msituni kuchimba dawa na kisha kurudi nayo na kuingia kilingeni kwake ila gafla akamuona Neema akiwa ndani ya kilinge cha yule mganga ambapo yule mganga alipoingia tu Neema alimpulizia kitu na yule mganga kuanguka chini na kutapatapa mwishowe akafa, kwakweli Sophia alishtuka sana na kuanza kuhemea juu juu na kumfanya Ibra nae aamke huku akimshangaa m,ke wake ambaye aliamua kumueleza vile alivyoota.
“Kheee inamaana Neema ndio amemuua huyo mganga?”
“Ndio hivyo mume wangu”
“Basi inaonyesha Neema ana nguvu sana au unaonaje?”
“Ni ana nguvu kweli mume wangu, tunachotakiwa kufanya ni kumtii tu.”
“Kwahiyo tutakuwa tunalala na kuamka kwa siku tatu bila ya kutoka nje duh!”
“Hakuna namna Ibra, yatupasa kufanya hivyo tu yani hakuna jinsi yoyote tumtii tu”
Wakakubaliana kuwa hawatotoka hadi hizo siku tatu alizozisema Neema ila Ibra akakumbuka kile alichokiona chooni,
“Hivi na haya mauza uza je yataisha?”
“Huenda yakaisha”
Wakasikia Neema akiwaita sebleni na kuamua kwenda kwani sasa walishauriana kuwa wapole na kufata kila wanachoambiwa na Neema ili iwasaidie kumuepuka baada ya hizo siku alizosema kuwa ataondoka.
Walimkuta Neema sebleni ambapo walipokaa tu Neema akaanza kuwaambia,
“Hongereni sana”
“Hongera ya nini tena Neema?”
“Sophia ni mjamzito”
Sophia na Ibra wakatazamana kwani wala hawakuwa na wazo kuwa Sophia ana mimba kwasasa, kisha Ibra akamuuliza Neema
“Umejuaje kama Sophy ni mjamzito?”
“Nilishakwambia kuwa mimi najua vitu vingi sana kwa kumuangalia mtu tu, na kama mnampenda huyo mtoto wenu basi mnatakiwa kusikiliza kile ninachowaambia mimi”
Ibra akamuangalia mke wake na kumwambia,
“Hongera sana mke wangu”
Sophy akatabasamu huku sura yake ikiwa imejawa na uoga, Neema akamuangalia Sophia na kumwambia,
“Kizazi chako kipo karibu sana hata ukiamua kuzaa watoto ishirini huwezi kushindwa ni maamuzi tu si unaona mwenyewe jinsi ilivyo fasta yani unatoa kitu unaweka kitu kwahiyo hata zile mimba zako zilizotoka zisikusikitishe sana”
Ibra akasema,
“Hata kama, ila bado tumepoteza watoto wetu wawili ambao huenda tungekuwa nae hata mmoja wapo humu tukicheza cheza nae”
“Msijali, mtoto mtampata tu na mtampenda sana kwani atakuwa tofauti na watoto wengine mliowazoea”
Ibra na Sophia wakatazamana huku wakiwa na hamu ya kumpata huyo mtoto wa tofauti na wengine kwani hawakuelewa huo utofauti ni kivipi, kisha Neema aliondoka pale na kuwaacha wakiwa wamekaa pale pale sebleni hadi muda wa kulala ulipofika.
Zilipita siku mbili bila ya wao kutoka nje wala kula na hawakuhisi njaa ya aina yoyote ile kwani muda mwingi walijihisi kushiba na hata hawakuelewa kwanini imekuwa vile na wala hawakujiuliza kuwa kwanini hawakuweza kula chakula.
Leo walipigiwa simu tena na Siwema ambaye alikuwa anasikitishwa tu na kile walichofanya,
“Yani mmeshindwa kabisa kuja hata kwenye mazishi? Mna matatizo gani nyie? Yani mmefanya kila mtu aamini kuwa nyie ndio chanzo cha mambo yote”
“Siwema huelewi tu kilichotoke ila kwasasa naomba tutulie, tutazungumzia hayo mambo siku nyingine”
“Yani mimi ninachotaka kuwaambia sasa ni kuwa msinisumbue tena kwa swala lolote lile, msiniambie kitu chochote sijui mambo mambo gani yamewapata msiniambie kwani sitajishughulisha kabisa kuwasaidia. Mmefanya mimi nionekane mtu mbaya huku yani nyie sina hamu kabisa kwa mliyonifanyia”
Ibra alimshangaa tu Siwema kwani hakuona umuhimu wa wao kuwa msibani wala nini, ila Siwema alionyesha kukasirishwa sana na alikata ile simu kwa hasira. Ibra akamuangalia mke wake na kumwambia,
“Kwani sisi tungeenda huko msibani ndio tungemfufua huyo mzee?”
“Huyo Da’Siwema naye ana matatizo yake tu, kwahiyo anasema tusimueleze tena yani anajiona kama yuko peke yake dunia nzima wa kutusaidia loh!”
“Achana nae mke wangu”
Muda kidogo simu ikaita tena, Ibra akapokea na kusikia kuwa anaeongea upande wa pili alikuwa ni Lazaro,
“Ibra ndugu yangu naomba unisikilize kwa makini, Mungu anakupenda sana unatakiwa utoke kwenye hiko kifungo ulichofungwa na shetani. Jihurumie ndugu yangu Ibra, tafadhari kama hutojali naomba tuonane leo uje na mke wako nikupeleke kwenye maombi”
“Umemaliza?”
“Jamani Ibra kwanini unakuwa hivyo ndugu yangu jamani, hivi unajua kama ufahamu wako umeshikwa na shetani? Nimeota ndoto mbaya sana kuhusu wewe na sitaki kuona ukisumbuka ndugu yangu, wakati ni leo na ni sasa”
“Nimekuuliza hivi, umemaliza?”
“Nimemaliza ndio, natumaini utakuja tuonane ili tujue tunapoanzia kukusaidia maana swala la imani ni wewe kuwa na utayari huku ukimuamini Mungu”
“Haya kwaheri, halafu jifunze kufatilia maisha yako umesikia eeh! Maisha yangu hayakuhusu, maana umeona nimekaa kimya kwa kitendo chako cha kutembea na mke wangu umeniona mjinga, sasa sitaki upuuzi wako”
“Ila Ibra mimi sijatembea na mke wako, muulize vizuri akwa……..”
Ibra akakata ile simu na kumuangalia mke wake kisha akamwambia,
“Yani huyu Lazaro anataka kunikumbushia kidonda kilichoanza kupona”
“Jamani mume wangu, achana nae huyo”
“Hadi nina mashaka kuhusu hiyo mimba yako Sophy huenda ni yake”
Sophia akainama chini huku akitamani kumwambia Ibra ukweli kuwa hakutembea na Lazaro ila alishindwa jinsi ya kumueleza ukizingatia kwamba alishamtengenezea uongo kuwa kweli alitembea nae.
“Naomba nisamehe mume wangu, ila huyu ni mtoto wako”
“Akizaliwa tunaenda kupima”
“Jamani mume wangu kitanda hakizai haramu”
“Halafu wewe Siphy niondolee upuuzi wako na wewe, usifikiri kukukubali uone mie mume bwege nina akili zangu timamu kabisa sasa ukae kimya kabisa maana naweza kubadilika siku yoyote”
Ikabidi Sophia awe mpole kwani hakuweza kubishana na mume wake zaidi.
Ilipopita siku ya tatu Ibra alijihisi kupumua kwasasa kwani hakuweza kufikiria kama siku zote hizo waliweza kuvumilia kwa kukaa mule ndani bila ya kwenda mahali popote pale,
“Haya sasa mke wangu tumeshatoka kifungoni, sehemu gani ya kwanza ungependa twende?”
“Napenda twende hospitali kwanza ili nikahakikishe kama kweli nina mimba”
“Sawa ni jambo jema sana”
Wakajiandaa na kutoka ndani kwao ambapo waliingia kwenye gari yao na kuanza kuzungumza mambo mbalimbali,
“Hivi ndio kusema Neema kaondoka kweli?”
“Ndio ameshaondoka si unaona nyumba tulivyoiacha kimya na wala hajaonekana tangia jana jioni”
“Khee bora tupumue jamani”
“Kweli kabisa, tutaishi kwa amani sasa mke wangu na tukome kuhitaji wasaidizi wa ndani”
“Kuhitaji wasaidizi sio kosa mume wangu ila kosa ni kuokota okota hao wasaidizi”
Wakacheka kwa pamoja, wakafika hospitali na kushuka kisha kuelekea kwa daktari moja kwa moja.
Baada ya vipimo wakaletewa majibu na kupewa hongera kuwa Sophia ni mjamzito,
“Muwe makini sana kwasasa, napendekeza uanze kliniki mapema ili tuwe tunajua maendeleo ya mtoto”
“Sawa, kwahiyo naweza kuanza kliniki lini?”
“Unaweza kuanza hata wiki ijayo kisha utakuwa unakuja kila mwezi ili tuangalie maendeleo yako na mtoto”
“Nimekuelewa dokta nitakuwa makini sana kwasasa”
“Itakuwa vizuri”
Wakaagana na daktari pale kisha kuanza safari ya kurudi nyumbani kwao huku wakiwa na furaha sana.
Walipofika nyumbani waliingia ndani na kweli nyumba ilikuwa kimya sana ila gafla wakasikia sauti ya mtoto akilia,
“Mmh hiyo sauti inatokea wapi?”
“Kama hapo nje kwetu”
Ikabidi watoke ili wakaangalie kuwa kuna nini, walipofika nje sauti ile iliongezeka na ilionekana kutokea kwenye gari yao na kufanya wasogelee gari huku wakiwa na mashaka sana.
Wakasikia kama sauti ikitokea kwenye buti la gari na kufanya Ibra aamue kufungua, wakashtuka sana kumkuta mtoto mchanga ndani ya buti hilo akiwa ameviringishwa na khanga huku pembeni yake kukiwa na barua iliyowashtua sana.
Itaendelea kama kawaida………..!!!!
NYUMBA YA MAAJABU: 32
Ikabidi watoke ili wakaangalie kuwa kuna nini, walipofika nje sauti ile iliongezeka na ilionekana kutokea kwenye gari yao na kufanya wasogelee gari huku wakiwa na mashaka sana.
Wakasikia kama sauti ikitokea kwenye buti la gari na kufanya Ibra aamue kufungua, wakashtuka sana kumkuta mtoto mchanga ndani ya buti hilo akiwa ameviringishwa na khanga huku pembeni yake kukiwa na barua iliyowashtua sana.
Ibra aliichukua ile barua na kuanza kuisoma kwa makini kwani maneno yake yalikuwa machache sana na yaliyoeleweka.
“Najua mnapenda sana watoto, tafadhari nawaomba mumlee mtoto huyu mfanyeni kama mtoto wenu make nae vizuri. Msimfokee na wala msithubutu kumpiga, tafadhari sana msimtupe mtoto huyu. Asante”
Ibra akatazamana na mke wake kwani ilikuwa ni kitu cha ajabu kilichowapa maswali mengi sana kwani walijiuliza kuwa ni nani anaweza kuwawekea mtoto kwenye buti la gari ila wakakosa jibu, wakati wakitafakari hilo yule mtoto alianza kulia tena na kumfanya Sophia huruma imjae na kumuinua yule mtoto kisha kuelekea ndani huku akifatwa na mume wake, Sophia alifanya kazi ya kumbembeleza yule mtoto na kuhisi kuwa huenda ni njaa iliyomfanya alie vile,
“Inatakiwa tumtafutie maziwa mume wangu”
“Itabidi tufanye hivyo, ngoja nikaangalie madukani huko”
Ilibidi Ibra atoke na kumuacha Sophia akihangaika kumbembeleza yule mtoto ambaye alilia tu mfululizo bila kunyamaza na kumfanya Sophia ajihisi kama kuchanganyikiwa vile.
Ibra alienda dukani moja kwa moja na kununua maziwa pamoja na chuchu ya mtoto, wakati anatoka pale dukani kuna mmama wa makamo ambaye alikuwa ni mteja pia akamfata Ibra kwa nyuma na kumuuliza,
“Hayo maziwa unampelekea nani?”
“Si maziwa ya watoto haya! Nampelekea mtoto akanywe”
“Hebu chukua hilo kopo na uangalie hapo chini pameandikwa nini”
Ibra akachukua lile kopo na kuangalia kwa makini kisha kulisoma,
“Maziwa ya mama ni bora zaidi”
“Eeeh kwanini ukampe mtoto maziwa ya kopo badala ya maziwa ya mama?”
“Aaah-mmh-aaah unajua aaah-mmmh”
“Mbona unajiuma uma, nini tatizo? Kwanini msimpe mtoto maziwa ya mama? Unajua madhara ya maziwa ya kopo wewe?”
Ibra akatikisa kichwa kuwa hajui, kisha akajitetea,
“Unajua sisi mtoto mwenyewe tumemuokota tu”
“Hata kama mmemuokota, mtoto wa mwenzio ni sawa na mtoto wako, kwanini umpe vitu ambavyo havifai mtoto wa mwenzio?”
“Sasa hayo maziwa ya mama tutayatoa wapi? Na hata hivyo, kama haya maziwa ni mabaya mbona yanauzwa?”
“Hivi si unazijua sigara wewe? Zinauzwa na pale chini zimeandikwa onyo uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako ndio hivyo hivyo kwa hayo maziwa, umesoma mwenyewe hapo kuwa maziwa ya mama ni bora zaidi, haya sasa jiulize kwanini umpe mtoto maziwa ya kopo na sio maziwa ya mama? Unataka mtoto awe tahira? Je unataka awe zezeta useme amerogwa kumbe sababu ya miziwa ya kopo hiyo, unataka mtoto awe mjinga?”
“Ila mbona kuna watoto wengi tu nawafahamu wamekulia maziwa ya kopo na hawako hivyo?”
“Nisikilize mimi ni mtu mzima, sijakurupuka kukufuata na kukwambia kuhusu hayo maziwa, wenzenu ni wafanyabiashara tu shauri yako. Narudia kukwambia maziwa ya mama ni bora zaidi”
“Sasa mimi nitafanyaje ikiwa mtoto mwenyewe tumemuokota?”
“Memuokota ndio, je huna mke wa kumnyonyesha huyo mtoto?”
“Mke wangu hajazaa bado”
“Hata kama mkeo hajazaa, kila mwanamke anaouwezo wa kunyonyesha, kuna vitu tu vya kumpa ale kisha maziwa yanamtoka na ananyonyesha kama kawaida”
“Ila hata hivyo mke wangu ni mjamzito”
“Kumbe mkeo ni mjamzito, sasa si ndio vizuri hivyo. Hujui kama wajawazito huwa wanatoka maziwa? Ukifika nyumbani mwambie mkeo akamue chuchu zake uone maziwa yanavyotoka, mnyonyesheni mtoto huyo mtamuharibu akili kwa hayo maziwa ya kopo”
“Sasa mwanamke mjamzito ananyonyeshaje jamani, kwani wanaruhusiwa?”
“Kwanini wasiruhusiwe? Kama ameweza kubeba kiumbe tumboni atashindwaje kunyonyesha kiumbe anachokiona? Mshauri mkeo amnyonyeshe huyo mtoto, acheni kumnyanyasha m,toto mdogo mnamnyima haki yake’
Ibra akamshukuru yule mama kisha kuingia kwenye gari yake na kuanza kurudi nyumbani huku akitafakari mambo m,engi bila hata ya majibu.
Aliupofika nyumbani alikuta yule mtoto bado akilia huku Sophia akihangaika kumbembeleza,
“Kheee jamani hajatulia toka muda ule?”
“Mwenzangu yani anatulia kidogo na kuanza tena kulia, huyu mtoto ni balaa. Lete hayo maziwa nikamtengenezee”
Ibra akamkabidhi mkewe yale maziwa ambapo aliyakoroga na kungoja yapoe ili amnyweshe yule mtoto ila muda huo alitulia kidogo kisha Obra akaanza kumwambia mkewe kuhusu hoja alizopewa na yule mmama aliyekutana nae dukani.
“Kheee yani nimnyonyeshe maziwa yangu mimi?”
“Ndio, nasikia ndio vizuri inamsaidia mtoto kuwa na nguvu na afya zaidi eti hayo maziwa ya kopo hayafai”
“Sasa mimi nitamnyonyeshaje wakati ni mjamzito?”
Ibra akamwambvia mkewe ajaribu kutoa ziwa lake na kulikamua ambapo Sophia akafanya hivyo na alipokamua kweli chuchu zake zikatoa maziwa,
“Eeeh si unaona kuwa maziwa yanatoka? Kwamaana hiyo una uwezo wa kumnyonyesha huyu mtoto”
“Ila kwa nijuavyo mimi, mwanamke ukiwa mjamzito huruhusiwi tena kunyonyesha. Nakumbuka hata dada yangu Rehema alipombebea mimba mtoto wake ilibidi amuachishe ziwa mara moja sasa hizo habari za kuniambia kuwa naweza kumnyonyesha mtoto ingawa nina mimba nazishangaa sana”
“Usishangae Sophia nimeshauriwa na mtu mzima kabisa, ni mmama wa makamo yani haya mambo yote anayajua vizuri sana”
“Hata kama, kwakweli siwezi Ibra yani siwezi kabisa kumnyonyesha huyu mtoto wakati nina mimba tayari labda nishauriwe na daktari”
“Sophy usiwe mbishi kiasi hiko mke wangu, halafu kumbuka kuwa tumeambiwa tumlee huyu mtoto kama mwanetu kabisa kwahiyo tunatakiwa kumnyenyekea sana”
“Nimeshasema siwezi, Ibra siwezi”
Maziwa yale yalikuwa tayari kisha Sophia akachukua na kuanza kumpa yule mtoto ila alionekana kuyakataa kabisa yale maziwa na kuanza tena kulia, safari hii alilia sana hadi sauti yake ilianza kukauka,
“Sophy mke wangu mjaribishe na maziwa yako”
“Jamani Ibra kwanini hunielewi? Siwezi”
“Hivi kwanini wanawake mnakuwa na roho mbaya kiasi hiko jamani Sophy! Hivi huna huruma hata kidogo kwa jinsi mtoto huyu anavyolia? Si unataka watu wajae hapa na kutuuliza kuna nini jamani! Hebu kuwa na utu basi”
“Sasa maziwa yangu ndio atakunywa?”
“Mjaribishe tu, huwezi jua”
Sophia huruma ikamuingia na akajaribu kutoa ziwa lake na kumpa huyo mtoto ambaye alilidaka vizuri sana na kuanza kunyonya mpaka akapitiwa na usingizi ambapo Sophy akamlaza kwenye kochi pale sebleni.
“Haya sasa mke wangu umemeguka wapi kwa kumnyonyesha huyo mtoto?”
“Nisamehe bure mume wangu, mi nilijua haiwezekani”
“Hakuna kinachoshindikana, tulikuwa tunamtesa tu muda wote”
“Basi yaishe mume wangu”
Kisha Sophia akaenda jikoni kwa muda huo kuandaa chakula chao.
Sophia aliandaa chakula mezani na kumkaribisha mumewe ambaye alisogea pale mezani na kuanza kula ila leo walisifia sana kile chakula kwani kilikuwa ni kitamu kupiliza,
“Kwakweli leo mke wangu hiki chakula umekipika na kimepikika”
“Halafu nimekipika kawaida tu mume wangu”
“Hongera sana, chakula kitamu sana ndiomana nakupenda wewe”
Sophia akatabasamu na kumuangalia mumewe kwa furaha huku wakiendelea kula, walipomaliza tu kula yule mtoto nae akaanza kulia na kufanya Ibra na mkewe watazamane,
“Haya kamchukue mtoto”
“Unajua haya mambo hatujazoea”
“Ndio tunatakiwa tuzoee sasa, maana tukipata mtoto ndio hivi hivi”
Sophia akamchukua na kuanza kumbembeleza ila yule mtoto alikazana kulia tu, Ibra akamwambia mke wake
“Ukiona analia hivyo ujue anataka maziwa”
“Jamani kila muda?”
“Ndio kawaida ya watoto, hujui kwani? Mtoto anatakiwa kunyonya kila muda”
Ikabidi Sophia aanze tena kumnyonyesha yule mtoto ambapo alinyonya sana tu hadi Sophia mwenyewe akahisi maziwa yake yanauma, alipotulia alimuweka pembeni
“Duh huyu mtoto ananyonya hadi maziwa yananiuma”
“Ni kawaida ya watoto Sophy mke wangu utazoea tu maana na wetu huyo yupo njiani anakuja”
“Hata kama Ibra, ananyonya sana bhana”
Yule mtoto alikuwa ametulia kabisa muda huu ingawa alikuwa macho ila hakulia wala nini, walikaa pale na kuongea ongea mwisho wa siku wakakumbuka hoja ya kwa mjumbe,
“Hivi kuna umuhimu wa kumpeleka huyu mtoto kwa mjumbe?”
“Sasa mtoto mdogo hivi tumpeleke kwa mjumbe akatafute nini jamani? Kwakweli sioni umuhimu Ibra, kwa mjumbe inatakiwa tukimuokota mtu mzima kama yule Neema”
“Ila kweli mke wangu, kwa mjumbe inatakiwa tupeleke mtu mzima na sio mtoto mdogo hivi”
Wakajadiliana pale na mwisho wa siku wakakubaliana kuwa waende kulala.
Wakati wamelala, Sophia akajiwa na ndoto ya mtoto mmoja ambaye sura yake ilionyesha kusononeka sana kama kawaida Sophia alihitaji kumsogelea mtoto huyo ila kila aliposogea huyo mtoto nae akasogea mbele zaidi na mwishowe hakumfikia kabisa kisha akamuona yule mtoto akiishia kwa kumpungia mkono kama wa kumuaga Sophia.
Akajikuta akishtuka gafla kutoka usingizini huku akihema sana, mara gafla akajihisi maumivu ya tumbo chini ya kitovu kwakweli tumbo lile lilimuuma sana na kumfanya ahangaike pale kitandani kwa maumivu ila alipotaka kumuamsha mumewe hakuweza kwani hata huyo mumewe mwenyewe hakushtuka hata kidogo kwahiyo Sophia alikuwa akiugulia peke yake tu lile tumbo hadi panakucha ambapo Ibra aliposhtuka tu na maumivu ya tumbo kwa Sophy yalikata palepale na kumfanya Sophia abaki akijishangaa tu,
“Vipi mke wangu unajisikiaje?”
“Hivi unajua sijalala usiku wote”
“Kwanini? Mtoto alikuwa ananyonya sana?”
“Hapana mume wangu, huyo mtoto tangu tumlaze hapo hajaamka kabisa, yani usiku wote nilikuwa naugulia peke yangu tumbo limeniuma sana”
“Tumboo? Kheee pole sana mke wangu, kwahiyo saivi unajisikiaje?”
“Nashangaa tu hapa uliposhtuka wewe na tumbo nalo limeacha kuuma muda huo huo”
“Kheee mbona majanga sasa jamani, kwahiyo mimi ndio nilikuwa dawa? Vipi lakini hakuna hali nyingine yoyote maana hadi uoga umenishika”
“Hali gani kwa mfano?”
“Yani labda unatoka damu?”
“Hapana ni tumbo tu, natumaini mtoto wetu yupo salama”
“Nina hamu sana na huyo mtoto wetu naamini pia yupo salama, pole kwa kutokulala mke wangu jamani”
“Asante sana, vipi leo utaenda kazini?”
“Hapana siendi, nitaenda kesho leo nitakusaidia kulea”
Kisha Ibra akaamka na kuelekea sebleni ambako alikuta chai imeandaliwa mezani na kumfanya ahisi kuwa Sophia alishaiandaa kwahiyo akaenda pale mezani na kunywa ile chai kisha akaenda kukaa na kuanza kuangalia Tv.
Sophia nae alipotoka chumbani na kukuta chai mezani akajua mumewe ameand ile chai kwahiyo naye akaenda kukaa na kunywa ile chai kisha akamfata mumewe alipokaa na kumshukuru.
“Asante mume wangu kwa chai”
“Kheee natakiwa mimi nikushukuru wewe, au unanitega kwavile sijashukuru? Asante mke wangu kwa chai”
Sophia akamshangaa mumewe kwani alijua kuwa yeye ndiye ameandaa ile chai, ila kabla hawajaanza kujidadisi ikasikika sauti ya yule mtoto akilia na kumfanya Sophia aelekee chumbani.
Alimkuta yule mtoto pale kitandani ambapo Sophia alimuangalia kwa muda kidogo bila ya kumnyanyua, mara gafla akamsikia yule mtoto akisema,
“Masma nipe nyonyo ninyonye”
Sophia alishtuka sana.
Itaendelea kama kawaida……….!!!!!
Toa maoni yako mdau.
NYUMBA YA MAAJABU: 33
Alimkuta yule mtoto pale kitandani ambapo Sophia alimuangalia kwa muda kidogo bila ya kumnyanyua, mara gafla akamsikia yule mtoto akisema,
“Mama nipe nyonyo ninyonye”
Sophia alishtuka sana, akamuangalia kwa makini yule mtoto ambaye alirudia tena ile kauli yake,
“Mama nipe nyonyo ninyonye”
Sophia kwa uoga akatoka chumbani na kukimbilia sebleni ambako alimshtua mume wake na kumwambia huku akihemea juu juu,
“Ibra yule mtoto anaongea”
“Anaongea? Kivipi?”
“Anaongea kama kuongea, unajua kaniambia eti mama nipe nyonyo”
“Mmmh hebu acha masikhara Sophy, mbona unayoyasema hayawezekani?”
“Nenda kajishuhudie mwenyewe”
“Basi twende wote”
“Nenda tu, mi niache hapa hapa”
Ibra aliinuka na kuelekea chumbani ambako alimkuta yule mtoto akiwa amelala fofofo, Ibra akatikisa kichwa na kutoka hadi sebleni na kumuangalia mke wake huku akisema,
“Unajua wewe hujaacha mawenge mke wangu, haya huyo mtoto aliyekuwa anaongea yuko wapi wakati mtoto amelala yule”
“Amelala? Huyo mtoto atakuwa ni muongo mume wangu maana mi nimeshuhudia kwa macho yangu akiongea”
“Hivi Sophy unawezaje kumuita malaika ni muongo? Au hujui kama mtoto ni malaika?”
“Sio kwa malaika yule, mi siwezi hata kulala nae leo.”
Ibra akahisi kuwa mkewe matatizo yamemrudia tena ndiomana anakuwa hivyo ila akajaribu kuzungumza nae ili aweze kumuweka katika hali salama lakini Sophia alionekana kuwa mgumu sana kuelewa mpaka pale Ibra alipoendelea kumsisitiza kuwa itakuwa ni ndoto tu.
Muda huu Ibra alijiandaa na kumuaga mke wake kuwa anatoka kidogo, kwani alihitaji kwenda kuonana na Jane ili aweze kumueleza kuhusu yule mtoto waliyemuokota na kusikiliza ushauri wake kuwa atamwambia afanye nini kwani alikumbuka alivyomshauri kwa Neema kuwa aende kwa mjumbe sasa alihitaji kujua na kuhusu huyu mtoto atamwambia nini.
“Tafadhari Ibra usitoke na kuniacha peke yangu”
“Kwani tatizo ni nini jamani Sophia? Kwahiyo hatutafanya tena kazi?”
“Sio hivyo mume wangu ila nakuomba usitoke kwanza, ngoja tuzoee pamoja kuishi na huyu mtoto”
“Kheee makubwa haya, mtu mzima atusumbue akili halafu leo hii mtoto nae atusumbue akili? Unataka tukamtupe mtoto huyu? Hebu fikiria mimba uliyobeba, hebu jaribu kuwa na uchungu kama mama. Fikiria mimba zilizotoka, fikiria maumivu uliyopitia ndio umuwazie mabaya huyu mtoto”
“Sikia Ibra, mimi sina nia mbaya na huyu mtoto ila tu sijisikii vizuri kubaki nae peke yangu. Naomba tubaki wote”
“Nimekuuliza, je tutakuwa hatufanyi kazi? Je maisha yetu yataendeshwa na kitu gani? Hebu fikiria hilo kwanza mke wangu, mimi leo sitatoka ila fikiria kwa makini jinsi maisha yetu yanavyoenda”
Sophia hakujibu kitu chochote, mara akasikika yule mtoto akilia huku Sophia akiogopa kwenda kumchungulia wala kumchukua, ikabidi Ibra ainuke na kwenda kumchukua yule mtoto na kutoka nae sebleni kisha akamuomba Sophia amnyonyeshe yule mtoto,
“Naogopa bhana”
“Sophia, umeitoa wapi hiyo roho mbaya? Kwani maziwa hayo unalipia bili jamani? Hayo maziwa ni bure tu sasa unashindwa nini kumnyonyesha mtoto?”
“Mtoto mwenyewe ananyonya sana”
“Hata kama ananyonya sana, si utakula chakula kwani tatizo liko wapi jamani mke wangu? Tunapomfanyia mabaya mtoto huyu tunatakiwa kwanza tufikirie kwa makini kuhusu mtoto wetu ajae.”
Sophia hakujibu kitu ila akamchukua mtoto yule na kuanza kumnyonyesha ambapo alinyonya kwa masaa kama mawili mpaka Sophia akaanza kulalamika kuwa maziwa yanamuuma sana, yule mtoto akatabasamu na kuacha kunyonya kisha akalala.
Ibra akampa pole mke wake na kumwambia kuwa anatakiwa kuwa mvumilivu.
“Hata hivyo Ibra, ila kwanini huyu mtoto ananyonya sana?”
“Mbona ni kawaida ya watoto Sophia”
“Unajua Ibra nimeshaishi na watoto wengi tu ingawa sijawahi kulea mtoto wangu mwenyewe ila naweza kujua jinsi ukuaji wa watoto ulivyo. Kwa nijuavyo mimi ni kuwa watoto wa kiume wanakula sana ila hawamfikii huyu mtoto, hata hivyo huyu ni mtoto wa kike iweje awe anakula kiasi hiki? Akiendelea hivi nampa uji au ugali kabisa”
“Sophia jamani mbona unakuwa hivyo? Wewe ulilishwa ugali wakati mdogo? Kwanini sasa umuharibu utumbo huyu mtoto?”
“Halafu kwanini unamtetea hivi huyu mtoto, kwanini mume wangu?”
“Unajua nini Sophia, tushapoteza watoto wetu wengi tu kwahiyo nikimuona huyu mtoto huwa naona kama mwanangu vile ndiomana namuhurumia sana”
Sophia alimuangalia tu mumewe bila ya kuongeza neno kisha akamlaza yule mtoto pale kwenye kochi.
Wakapitiwa na usingizi wote pale ndani kwao, yani hakuna ambaye alikuwa macho kwa muda huo. Sophia akajiwa na ndoto amapo katika ndoto ile alijiona akiwa na mumewe chumbani huku mumewe akimwambia,
“Sophy mke wangu ukizaa huyo mtoto namuua”
“Kheee kwanini umuue sasa jamani?”
“Lazima nimuue, kwakweli siwezi kukubali tupate mtoto mwingine wakati tuna mtoto tayari. Na vile vile mtoto mwenyewe huyo sina uhakika kama ni mtoto wetu kweli”
“Una kichaa au? Tuna mtoto tayari! Mtoto yupi jamani, au unamuongelea huyu tuliyemuokota?”
“Ndio, huyu mtoto anatutosha kabisa. Sasa ole wako umzae huyo mtoto au huamini kama nawaza kumuua?”
“Siamini na kamwe siwezi kuamini”
Gafla akamuona Ibra akimpiga teke la tumbo na kumfanya Sophia ashtuke sana kutoka kwenye usingizi ule huku akihemea juu juu na kumuamsha Ibra,
“Ibra, Ibra nimeota ndoto mbaya sana”
Ibra aliamka huku akiwa haelewi elewi, na kumuuliza mkewe
“Umeota ndoto mbaya kivipi jamani?”
“Yani, nimeota kuwa dah hata sijui nisemeje”
“Hebu niambie ilivyokuwa niweze kuelewa”
Sophia akamsimulia mumewe jinsi alivyoota huku akishika tumbo lake, Ibra akamsogelea mkewe na kumkumbatia kisha akamwambia,
“Sophy mke wangu, hiko kitu ulichoota hakipo yani hakipo kabisa kabisa sio kwa uhalisia wala kwa ndoto. Nakupenda mke wangu na pia napenda uzao wako. Watoto ndio furaha yetu na ndiomana tunafanya jitihada zote kuwapata sasa nawezaje kuanza kupinga uwepo wa mtoto wetu eti kwavile kuna mtoto tulimuokota tupo naye ndani? Huyu mtoto namjali na kumthamini kwavile natumai na sisi tutapata mtoto wetu kwahiyo hatutakiwi kumtenda vibaya mtoto huyu tutalaaniwa bure”
“Nashukuru kwa kunipa moyo mume wangu yani sitaki kumpoteza mtoto wetu huyu”
Sophia alikuwa akilishika shika tumbo lake huku akiliangalia kwa makini sana, ila walikaa pale bila ya kuhisi njaa wala nini yani si Sophia wala si Ibra hata wakawa wanashangaa tu,
“Sophy si unanyonyesha wewe yani na wewe huna njaa?”
“Hata nashangaa yani njaa imepotea kabisa, najihisi kushiba hatari”
Wakaamua kuendelea kujadili mambo mengine na kuachana na zile habari za njaa.
Muda kidogo sophia akaona ni vyema kuwa akamlaze yule mtoto chumbani sababu muda wote alilala hapo sebleni kwahiyo akambeba na kwenda kumlaza chumbani kisha yeye akarudi tena pale sebleni ila muda kidogo wakasikia hodi na kumfanya Ibra ainuke na kufungua mlango, alishangaa kuona mgeni mwenyewe ni Jane,
“Kheee Jane, nani amekufungulia geti?”
“Mbona geti lenyewe nimelikuta wazi jamani”
Akaingia ndani na kumsalimia Sophia ambapo leo aliitikia vizuri tofauti na siku zingine, baada ya ile salamu gafla mtoto wa chumbani akaanza kulia na kumfanya Sophia aende kumchukua na kurudi nae sebleni ambapo alipofika nae tu Jane akashangaa na kuuliza,
“Kheee kumbe mna mtoto jamani? Dada alikuwa na mimba kubwa? Mbona majuzi tu sikuwaona na mimba?”
Ibra akaamua amueleze ukweli kuwa yule mtoto wamemuokota na wameamua kumlea pia akamueleza mazingira waliyomkuta nayo huyo mtoto, kwakweli Jane aliwapongeza sana na kuwasifu kwa huo uamuzi wao,
“mmefanya jambo la maana sana, yani watu hawajui tu kama kulea watoto kama hawa ni vizuri”
“Ila changamoto iliyopo Jane ni kuhusu maziwa, yani huyu mtoto hataki maziwa ya kopo halafu vilevile Sophia nae hataki kumnyonyesha”
“Kheee dada jamani hebu acha hizo, yani mtoto mdogo hivyo unataka kumnywesha maziwa ya kopo? Sio mazuri yale, unatakiwa kumnyonyesha mtoto huyo ndio unampa nguvu na afya”
“Ila jane huyu mtoto ananyonya sana ndiomana inakuwa hivi”
“Kunyonya ni kawaida ya watoto dada yangu hata usishangae, unatakiwa kumpa maziwa mtoto kila anapohitaji wewe mnyonyeshe tu hata kama ananyonya kwa masaa matatu mfululizo mnyonyeshe tu”
“Bora umemshauri wewe, eeeh hivi mtoto huyu nae tumpeleke kwa mjumbe?”
Jane akacheka huku akiwajibu,
“Sasa mkimpeleka mtoto kama huyu kwa mjumbe si mtachekesha jamani, yani mtoto mdogo hivi eti mnampeleka kwa mjumbe inamaana mnaogopa kuibiwa au?”
“Ila hata mimi nilifikiria hilo na kuona kuwa halina umuhimu, kwakweli asante sana Jane kwa kuja”
Yule mtoto akaanza kulia tena na kumfanya jane amsisitize Sophia kuwa amnyonyeshe yule mtoto kisha akainuka na kuaga na kuondoka zake. Sophia alianza kumnyonyesha yule mtoto huku akizungumza na Ibra,
“Ila mbona kama leo Jane amebadilika sana?”
“Hata mimi mwenyewe namshangaa, yani kwajinsi anavyopenda kupinga yule binti yani lazima angetupinga kuhusu kumlea huyu mtoto ila cha kushangaza yeye ndio ametusapoti na kutupa nguvu zaidi”
“Kwakweli nimemshangaa sana, halafu leo sijamchukia kama siku zote eti nimempenda leo”
“Basi Jane kabadilika, tuwe tunamkaribisha. Mara ya mwisho naongea nae alianza kuniletea habari za mchungaji wao nikamshushua naona leo kajirekebisha”
“Alizidi sana, ila bora amebadilika kwakweli”
Ibra na Sophia waliongea kwa furaha sana muda huu huku yule mtoto akiendelea kunyonya.
Giza liliingia huku Sophia akiwa anaendelea kumnyonyesha yule mtoto na kumwambia mume wake,
“Nachoka Ibra nachoka sana, hebu ona masaa matatu sasa yamepita huyu mtoto ananyonya tu hivi kuna maziwa kweli humu au ananyonya damu jamani?”
“Pole mke wangu ila ndio uleaji mzuri huo, hukumsikia Jane alivyosema? Tunatakiwa kumnyonyesha sana huyu matoto bila kuchoka”
“Hivi unajua kama maziwa yananiuma kama yana vidonda vile?”
“Vumilia mke wangu jamani, kuwa mvumilivu”
Sophia akainuka na kwenda na yule mtoto chumbani ambapo baada ya muda kidogo tu yule mtoto alilala, kisha Sophia akatoka mule chumbani na kujikongoja hadi jikoni kwani muda huo njaa ilimshika sana kupita wakati mwingine, alipoingia jikoni alikuta chakula kipo tayari kwenye sufuria na kwavile njaa ilimshika sana hakuweza kuhoji kwahiyo aliamua kupakua na kuanza kula kule kule jikoni amabapo alikula na aliposhiba ndio aliinuka na kuelekea sebleni, ila kwa wakati huo ilionyesha kuwa Ibra alikuwa chumbani kwahiyo na yeye baada ya muda kidogo akaamua kwenda chumbani kulala kwani alimkuta Ibra akiwa amelala tayari.
Sophia alipopitiwa na usingizi akajiwa na ndoto, akamuona Neema nje ya nyumba yao na gafla yule Neema akageuka na kuwa Jane kisha akawagongea mlango na kuingia ndani. Sophia alishtuka sana na kuamka huku akishangaa, alikaa kitandani akitafakari kuwa Neema anawezaje kujigeuza na kuwa Jane? Na kwanini ajigeuze? Alikosa jibu kabisa ila aliogopa kumuamsha mume wake na kujipa matumaini kuwa ile ni ndoto tu kisha akarudi kulala.
Kulipokucha leo waliamshwa na sauti ya Yule motto akilia hivyo ikambidi Sophia aamke na kuanza kumnyonyesha Yule motto kisha Ibra nae aliamka na kwenda kuoga halafu akajiandaa kwaajili ya kutoka, akamuaga mkewe
“Vipi na leo tena hutoniruhusu kutoka?”
“Mmmh ngoja nifikirie kidogo”
“Ufikirie nini tena?”
“Nifikirie kuhusu kukuruhusu wewe”
“Tafadhali Sophia naomba niruhusu mke wangu maana nahitaji sana kujua kule dukani inakuwaje, hebu fikiria tangu lini hatujaenda kule. Naomba leo uniruhusu mke wangu”
“Sawa nakuruhusu ila tafadhali sana uwahi kurudi Ibra, usichelewe kama siku zote kumbuka nipo peke yangu”
“Haupo peke yako bhana upon a huyo motto”
“Hta kama, unadhani huyu motto atanisaidia nini sasa? Hapa ni sawa na kama nipo mwenyewe tu, tafadhali sana uwahi kurudi”
Ibra akamuahidi mkewe kuwa atawahi kurudi kwani hata yeye hawezi kumuacha ashinde mwenyewe kwa muda mrefu ukizingatia ana motto mdogo sana pale ndani.
Kama kawaida Ibra alitoka na kupanda gari yake kisha kuondoka pale nyumbani kwake, ila alipokuwa njiani akamuona Jane na kuamua kusimamisha gari ili amsalimie.
“Jane, za tangu jana?”
“Tangu jana? Kwani tumeonana na wewe jana kweli?”
“Si ulikuja nyumbani wewe!”
“Mmmh kaka labda kuna mambo unachanganya, mimi sijaja kwenu mud asana na hata hiyo jana sijaja kwenu sasa ni jana ipi unaiongelea?”
“Kheee wewe Jane jamani, si ulikuja na kuanza kutupa ushauri mule ndani jinsi ya kulea yule motto”
“Kwani mna mtoto? Dada kajifungua lini?”
“Unajua acha masikhara Jane, si nilikueleza jana kuwa mtoto tumemuokota”
“Mmemuokota? Je mmetoa taarifa polisi?”
“Unajua Jane usinichanganye tafadhali”
“Sikuchanganyi chochote ila wewe ndio unanichanganya mimi maana nashindwa kukuelewa”
Ibra hakuendelea kujadiliana na Jane bali aligeuza gari yake na kurudi nyumbani kwake ili akamuelezee mkewe vile alivyokutana na Jane na kukana kuwa hakwenda hapo jana.
Alipofika nyumbani alishangaa kuona kuna ukimya sana na kuhisi kuwa huenda Sophia na mtoto watakuwa wamelala, Ibra alifungua mlango na kukuta uko wazi tu,
“yani Sophy hakuinuka hata kufunga mlango!”
Akakumbuka kuwa alimuacha Sophia akimnyonyesha Yule mtoto, moja kwa moja akaenda chumbani, ila akashtuka sana kwani alimuona Sophia akiwa chini huku damu zikimtoka.
Itaendelea kama kawaida………!!!!!!!!
Toa maoni yako mdau.
NYUMBA YA MAAJABU: 34
Alipofika nyumbani alishangaa kuona kuna ukimya sana na kuhisi kuwa huenda Sophia na mtoto watakuwa wamelala, Ibra alifungua mlango na kukuta uko wazi tu,
“yani Sophy hakuinuka hata kufunga mlango!”
Akakumbuka kuwa alimuacha Sophia akimnyonyesha Yule mtoto, moja kwa moja akaenda chumbani, ila akashtuka sana kwani alimuona Sophia akiwa chini huku damu zikimtoka.
Ibra akahisi kuchanganyikiwa, akamtikisa mkewe pale chini alikuwa kimya kabisa na kumfanya Ibra apatwe na uoga kisha akamnyanyua mkewe na kumuweka begani halafu akatoka nae nje na kumuweka kwenye gari huku akielekea nae hospitali.
Walifika hospitali na kupokelewa amabapo moja kwa moja Sophia akapelekwa kwenye chumba cha huduma, Ibra alikuwa nje amechanganyikiwa kabisa hata akasahau kuwa nyumbani kwao kuna mtoto yupo ndani.
Muda kidogo daktari akamuita Ibra na kumuuliza maswali huku akijaribu kumueleza hali ya mgonjwa,
“Samahani ndugu, kwani huyu mgonjwa chanzo kilikuwa ni nini?”
“Hata sifahamu kwakweli, mimi nilimuacha nyumbani akimnyonyesha mtoto na niliporudi ndio nikamkuta na hali hiyo”
“Kwahiyo huyu ana mtoto mdogo?”
“Aaah aaah ndio tuna mtoto mdogo nyumbani”
“Halafu ndio alikuwa na mimba nyingine?”
“Aaah aaah ndio, kwani mimba yake inaendeleaje?”
“Kwa mlichomfanya huyu hakuna cha mimba inaendeleaje wala nini, kwa kifupi ni kuwa mimba ya huyu ilishatoka. Na ubaya zaidi ni kuwa kizazi chake kimeonekana kuwa na matatizo kwasasa”
Ibra alikaa chini kwanza kwani hakutegemea kupata habari kuwa mimba ya mke wake imetoka ukizingatia aliona kuwa kwa kipindi hiki watapata mtoto wao ukiacha na Yule waliyemuokota.
“Pole sana ndugu yangu, ila kwakweli mlichokuwa mkikifanya hakistahiki kwa mama mjamzito yani unajua kabisa huyu ana mimba halafu unamfanya mmnyonyeshe mtoto mwingine na wakati huo huo mnampa lishe hafifu hivi mlikuwa mnategemea nini kwa hali yake? Inaonyesha alianguka na aliangukia tumbo ndiomana akapata matatizo hayo, hata hivyo inaonyesha kuwa damu imepungua sana mwilini kwahiyo mnatakiwa kuwa makini sana vinginevyo mtakuja kumuongezea damu huyu”
Ibra alikuwa kimya tu akitafakari huku akiwa na matumaini ya kupona kwa mkewe ingawa alikuwa na uchungu wa kupoteza mtoto mwingine.
Muda ukapita kisha daktari akamuita tena Ibra na kumpa habari zaidi kuhusu mkewe,
“Unatakiwa uwe makini sana vinginevyo utampoteza huyu”
“Niwe makini kwenye kitu gani haswa?”
“Kuwa makini kwenye chakula kwa sana ili kumsaidia aweze kurudisha afya yake, hakikisha anapata mlo bora na kamili, mboga za majani na matunda visikosekane kwenye mlo wake”
“Sawa daktari, hilo sio tatizo kwangu kwani nahitaji mke wangu arejee kwenye afya yake”
Basi daktari akamwambia kuwa jioni atawapa ruhusa kwahiyo wataweza kurudi nyumbani na mkewe, Ibra alishukuru hilo kisha akatoka nje kwenda kumtafutia mkewe chakula na wala hakujisikia kurudi nyumbani kwa muda huo kwahiyo akaenda hotelini moja kwa moja kumtafutia hiko chakula.
Alifika hotelini na kuagiza chakula kwahiyo alikaa mahali akisubiri chakula hiko huku akiwa ameagiza soda ambayo alikuwa akinywa huku akisuburi wamalize kuandaa hiko chakula.
Kulikuwa na wadada wawili wamekaa pale hotelini wanaongea,
“Hivi unamkumbuka Neema?”
“Namkumbuka ndio aliwahi kuwa mfanyakazi wa hii hoteli”
“Ulisikiaga mazishi yake yalivyokuwa?”
“Mmmh nilisikia tu kuwa amekufa ila sikufika kwenye mazishi ila ni miaka imepita tangu afe”
“Yani mazishi yake haijawahi kutokea, kulikuwa na mambo ya ajabu mwanzo mwisho halafu kulikuwa na tetesi kuwa Neema alitembea na mwanaume wa ajabu na ndio aliyesababisha kifo chake. Ila jambo linalofanya nikumbuke mazishi yake ni kuwa, hivi majuzi kuna rafiki yangu kaniambia kuwa kamuona mtu kama Neema vilevile unajua nimeshtuka sana na nikikumbuka yale mazishi yake ndio nazidi kupatwa na uoga”
“Sasa uoga wa nini ndugu yangu, kwani kuna lolote baya ulilomfanyia Neema? Hata hivyo mi siamini juu ya mizimu ila naamini kuwa duniani watu ni wawili wawili kwahiyo huyo atakuwa kafanana tu na Neema acha uoga ndugu yangu mtu akifa amekufa”
“Weee najua hujui mengi sana kuhusu kifo cha Neema na ndiomana unasema hivyo, mi naogopa sana maana hata mimi nimehusika kutangaza kuwa kifo chake kilikuwa cha utata na kilisababishwa na mwanaume wa ajabu”
“Kumbe uoga huo ni sababu ya umbea wako pole sana”
Kimya kidogo kikatawala, kisha yule rafiki akamshtua mwenzie kwa kumwambia,
“Neema huyo”
Yani kile kitendo kilimshtua sana yule dada ila pia kilipasua moyo wa Ibra na akahisi ukimuenda mbio sana na uoga kumshika, mwisho wa siku wale wadada walianza kucheka sababu ya kutaniana ila walishangaa Ibra kuwa na hali mbaya sana ikabidi wamuombe msamaha kama wamemshtua na yeye.
“Kaka samahani sana, maana inaonyesha tumekushtua sana tusamehe tafadhali sisi tulikuwa tunataniana tu”
Ibra hakuweza hata kuwajibu kwajinsi moyo wake ulivyokuwa ukienda mbio, muda huo yule muhudumu wa chakula nae alikuwa amemletea kile chakula Ibra alichukua na kuondoka zake.
Alikuwa na mawazo sana huku akiendesha gari,
“Kama Neema waliyekuwa wanamuongelea ni yule tuliyeishi nae ndani je inamaana tulikuwa tukiishi na marehemu?”
Ibra alihisi kusisimka mwili mzima na kuamua kuachana na hayo mawazo kwa muuda.
Ibra alifika pale hospitali na kwenda kwa mke wake moja kwa moja kisha akampa kile chakula, kwakweli Sophia alikula kile chakula kamavile anakimbizwa na ilionyesha wazi kuwa alikuwa na njaa sana. Alikula mfululizo bila ya nkuongea chochote mpaka alipomaliza kile chakula, ndipo alipomuangalia mume wake na kumshukuru kisha akajilaza tena, kwakweli ile hali ilimshangaza sana Ibra na akazidi kumuhurumia mke wake na ndipo lile swala la mtoto nyumbani kwao likamjia,
“Mmmh yule mtoto nadhani atakuwa amelia leo hadi sauti imemkauka, na pia nadhani ni vyema kama mke wangu akiacha kumnyonyesha yule mtoto”
Gafla na yeye akasinzia pale pale pembeni ya mke wake. Dokta ndiye aliyefika na kuwashtua kwani jioni ilikuwa tayari imeshaingia, Ibra alishtuka huku akijishangaa kuwa imekuwaje hadin akapitiwa na usingizi kiasi kile, akamuamsha na mkewe ili wamsikilize dokta.
“Ibra, na wewe umelala kwa mgonjwa jamani, nimeshawaruhusu sasa mnaweza kwenda nyumbani”
Ibra akainuka na mkewe pale kisha wakatoka nje na kuelekea kwenye gari yao, walipopanda tu Ibra akamuuliza mkewe hali yake,
“Ila hali yako unaionaje kwasasa mke wangu?”
“Naendelea vizuri ila mwili umechoka sana”
“Pole mke wangu, yani hata ongea yako inaonyesha ni jinsi gani umechoka. Pole sana”
Ibra akaendesha gari hadi nyumbani ambapo Sophia alikuwa kimya njia nzima, walifika na kuingia ndani ambapo walikaa sebleni bila ya kwenda sehemu nyingine yoyote, Ibra aliamua kumuuliza vizuri mkewe kwani kupooza kule hakuelewa kabisa,
“Sophia unajua umepoa sana mke wangu, ingawa unaumwa ila umepoa sana hata sielewi nadhani kuna jambo linalokuchanganya zaidi”
“Sio jambo Ibra, kuna mambo mengi sana yanayonichanganya yani nahisi kupagawa kabisa”
“Pole sana mke wangu ila ni vyema tukashirikishana”
“Nawawaza wanangu, kwanini kila siku mimi ndio napoteza watoto? Kwanini jamani nabeba mimba zinatoka? Inaniuma sana Ibra yani sina raha kabisa”
Mara Yule mtoto wa ndani kwao akaanza kulia na kuwafanya washtuke, Ibra akajiuliza
“Kheeee kumbe huyu mtoto bado yupo!”
Kisha akainuka na kwenda kumchukua halafu akarudi nae sebleni, akamuangalia mkewe akamuona machozi yakimtoka
“Vipi Sophia nini tatizo mke wangu?”
“Tafadhali Ibra usinipe huyo mtoto nimnyonyeshe nakuomba sana usinipe”
“Huyu tutampa maziwa ya kopo leo hata usijali mke wangu”
Ibra akainuka na kwenda kumkorogea Yule mtoto maziwa ila walipompa kama kawaida aliyakataa kabisa,
“Mmmh tutafanyaje sasa mke wangu?”
“Mwache akiwa na njaa atakunywa tu”
Muda huu huyu mtoto alionekana kutulia ila alikuwa anawaangalia sana hata Ibra akashangaa kuwa imekuwaje.
Giza lilikuwa linaingia wakiwa pale pale sebleni huku Sophia akiendelea kusema kuwa anajihisi kuchoka sana,
“Hivi kwanza mke wangu niambie chanzo cha kuumwa kwako leo”
“Unajua toka ule muda nimeamka huyu mtoto alikuwa akinyonya yani muda wote ananyonya tu gafla nikahisi nguvu zikiniishia na kuamua kumuweka pembeni ila wakati nainuka nikaanguka chini na sikumbuki tena kilichoendelea”
“Pole sana, huyu mtoto hutomnyonyesha tena nisamehe mimi mke wangu. Huyu mtoto anakumalizia lishe kabisa na dokta kaniambia kuwa inabidi ule sana ili uwe salama kwahiyo huyu mtoto tutampatia maziwa ya kopo tu”
“Ila toka mwanzo nilikwambia swala hilo ila wewe Ibra ulikuwa mbishi sana ona sasa tumeshampoteza mtoto wetu kwa kuthamini watoto wa kuokota”
“Nisamehe mimi mke wangu tafadhali”
Sophia alimjibu mumewe kuwa ameshamsamehe ingawa bado anauchungu na ile mimba yake iliyotoka, kisha Ibra akamuomba mkewe kuwa wale kwanza ndipo wajiandae na kulala. Ibra alikuta chakula jikoni na wala hakuhoji sana zaidi ya kupakua kisha yeye na mkewe kula chakula hicho, walipomaliza kula Sophia aliamua kwenda kuoga ili aweze kulala, ila alipoingia bafuni alishtuka sana kwani alikuta damu imetapakaa kila sehemu.
Sophia alipiga kelele na kutoka nje,
“Nini tatizo mke wangu kuna nini?”
“Damu Ibra, damu zimejaa chooni”
“Damu? Zimetokea wapi tena?”
“Sijui ila damu zimejaa chooni Ibra”
Ibra akaamua kwenda kuangalia mwenyewe ila hakuona damu yoyote na kumwambia mkewe kuwa ni mawenge tu yalikuwa yakimsumbua kichwani kisha akaamua kwenda kuoga naye pamoja.
Walipomaliza kuoga walimkuta Yule mtoto ameshalala, wakatazamana na kuulizana
“Inamaana huyu mtoto leo atakula nini?”
“Atakunywa hay ohayo maziwa njaa ikimshika vizuri”
“Hivi unajua kama ni toka asubuhi hajala chochote?”
“Unataka tufanyaje sasa mume wangu jamani, kama kula hataki tusubiri tu muda njaa ikimshika vizuri atayanywa hayo maziwa”
Wakakubaliana hilo kisha na wao kupanda kitandani na kulala.
Wakiwa wamelala, Sophia alihisi maziwa yakimuuma sana na kumfanya aamke kisha akakaa kitandani na kuangalia maziwa yake ambapo alishangaa ziwa moja likivuja maziwa na linguine likivuja damu kwakweli akapatwa na uoga kisha akamuangalia Ibra na kuanza kumuamsha ila kabla Ibra hajaamka Sophia alijishangaa akipatwa na usingizi pale pale na kulala, tena safari hii alilala fofofo kushinda mwanzo yani hakuweza hata kujigeuza.
Usiku wa manane Ibra nae akashtuka kutoka usingizini na moja kwa moja akamtazama mke wake ila alichokiona kilimshtua sana, alimuona mkewe akiwa kalala chali huku Yule mtoto akiwa juu ya mkewe ananyonya.
Itaendelea kama kawaida……..!!!!!!!!!!!
Toa maoni yako mdau.
NYUMBA YA MAAJABU: 35
Usiku wa manane Ibra nae akashtuka kutoka usingizini na moja kwa moja akamtazama mke wake ila alichokiona kilimshtua sana, alimuona mkewe akiwa kalala chali huku Yule mtoto akiwa juu ya mkewe ananyonya.
Ibra alijifikicha macho kwani alihisi kamavile haoni vizuri ila bado alipoangalia alimuona yule mtoto akikazana kunyonya, Ibra alisogea ili ajaribu kumtoa yule mtoto pale kifuani huku roho nyingine ikimwambia kuwa labda mtoto ana njaa sana ndiomana imekuwa vile ila akajiuliza kuwa hata kama mtoto yule ana njaa sana je pale kifuani amewekwa na mke wake au imekuwaje? Maana yule mtoto ni mdogo sana na ni ngumu kufanya vile. Akajaribu kumtoa sasa ila yule mtoto alionekana kulishikilia ziwa vilivyo kwa mdomo wake na kumfanya Ibra ashindwe kumtoa, akajaribu kumuamsha mke wake ila alishtukia akipigwa kibao na mtu asiyemuona, kibao ambacho kilipelekea aanguke kitandani na kupitiwa na usingizi pale pale.
Ibra alikuja kushtuka tena wakati kumeshakucha kabisa na bado alimuona yule mtoto akiwa pale pale juu ya mkewe akinyonya, Ibra alishtuka sana na uoga ukaanza kumuingia sasa akajikuta akitetemeka huku akiita,
“sophia, Sophia mke wangu, Sophia”
Ila Sophia alikuwa kimya kabisa huku amelala chali vile vile na yule mtoto akiendelea kunyonya, Ibra akajivika ujasiri sasa na kuamua tena kumtoa yule mtoto ila safari hii alifanikiwa na kumuweka kitandani, kale katoto kalikuwa kakimuangalia tu Ibra kisha Ibra akaanza kumuamsha tena mkewe ambaye alichukua muda mrefu sana kuamka na alionekana kutokuwa na nguvu kabisa kwani hakuweza hata kuitika vizuri, kwakweli Ibra huruma ilimuingia sana na kumpa pole mkewe ambaye hata kujibu hakuweza ila aliishia kumuangalia Ibra tu.
“Sophy, tafadhali tutoke twende hotelini ukanywe supu maana nikisema tutapika muda huu itakuwa uongo mke wangu”
Sophia aliitikia kwa kichwa tu kwani alionyesha kuzidiwa na njaa, ikabidi ibra amsaidie mkewe kuvaa kisha akaanza kumkongoja kutoka naye pale ndani hadi nje ya geti kisha safari ya kwenda hotelini ikaanza.
Walipofika hotelini moja kwa moja Ibra akamsaidia mkewe kushuka kisha wakaenda kukaa na kumuagizia supu ambapo ilipofika Sophia alikunywa kamavile anakimbizwa kwakweli ilionyesha ni wazi kuwa Sophia alikuwa na njaa sana, Ibra alikuwa akimuangalia mkewe huku akisikitika tu. Alipomaliza ile supu ikaletwa nyingine ambapo aliinywa pia kisha akaanza kurudi kwenye hali ya kawaida, Ibra akampa tena pole mke wake
“Pole sana Sophy”
“Asante”
“Hivi yule mtoto ni vipi ukaanza kumnyonyesha tena usiku wakati tulikubaliana kuwa usimnyonyeshe tena?”
“Yani hata mimi mwenyewe nashangaa, unajua nimeshtuka usiku na kumkuta yule mtoto akinyonya yani kapandaje kifuani pangu sijui. Angekuwa ni mtoto labda wa miezi hata mitano ningesema anauwezo huo sababu amekua kua ila sio kwa yule mtoto jamani, basi nikajaribu kumtoa nikashindwa na nguvu zikaniisha kabisa huku yeye akiendelea kunyonya yani muda unaniita nilikuwa nasikia ila nashindwa kuitika”
“Dah pole sana mke wangu, unajua hii okota okota yetu ndio inatuponza kwakweli sasa tufanyaje juu ya yule mtoto na kumbuka tumeambiwa kuwa tusimtupe”
“Unajua mimi sina imani kabisa kama yule ni mtoto kama watoto wengine, yule mtoto sio wa kawaida na ananipe mashaka mume wangu kwakweli sitawea kulala tena mule chumbani kwa uwepo wa yule mtoto”
Ibra akafikiria kidogo kisha akamuuliza mkewe,
“Unaonaje yule mtoto tuwe tunamlaza chumba alichokuwa analala Neema?”
“Labda tufanye hivyo kwakweli maana siwezi kabisa kuendelea kukubaliana na hii hali, yani hadi nimepata wazo la kurudi nyumbani kwetu”
“Hapana usifanye hivyo mke wangu, hebu nifikirie mimi unadhani nitawezaje kuishi peke yangu jamani! Tafadhali sophy mke wangu usifikirie huko, yule mtoto tutaanza kumlaza chumbani kwa Neema na hatotusumbua tena”
“Sawa, ila pia naomba hili swala la mimi kutoka maziwa likome mara moja maana ningekuwa sitoki maziwa basi yule mtoto asingekuwa anapata cha kunyonya toka kwangu. Sijui utanisaidiaje juu ya hili?”
“Hilo sio tatizo mke wangu tutajua tu cha kufanya ila kwasasa tumalizane kwanza na huyu mtoto maana naona kabisa lengo lake ni kukuua mke wangu. Hivi ni mtoto gani yule maana pale alipo hana hata mwezi mmoja halafu anafanya vituko kiasi hiki, nimemchoka kwakweli”
Wakapanga pale na kufikia muafaka wao kuwa yule mtoto wataanza kumlaza kwa Neema maana Ibra alihisi kuwa yule mtoto anaweza kuzidi kummaliza nguvu mke wake.
Walipomaliza pale wakaanza safari ya kurudi nyumbani ndipo Ibra alipokumbuka lile tukio la kukutana na Jane na jinsi Jane alivyoshangaa alipoambiwa kuwa alifika nyumbani kwao,
“kheee kwahiyo Jane kakataa kuwa sio yeye?”
“Yani kakataa kabisa”
“Mmmh sasa mbona naanza kupatwa na uoga jamani? Alikuwa nani sasa aliyekuja kwa sura ya Jane kiasi kile?”
“Hata mimi nimekosa jibu ila Jane amekataa kabisa kuwa yeye hakuja nyumbani kwetu”
“Ila hata siamini labda kama Jane kaamua kutufanyia mchezo tu mume wangu, hivi unamuaminije Jane jamani?”
“Sio namuaminije, kuna vitu Jane huwa anaongea ukweli mtupu kama unakumbuka alivyotuambia kuhusu Neema, iweje tusimuamini? Mimi naamini kuwa hakuwa yeye ingawa sijui sasa alikuwa ni nani”
“Maajabu hayo ila bado siamini kwakweli, yani mtu mweingine ajibadilishe na kuwa Jane halafu aje nyumbani kwetu na kuongea vile kweli? Ila nilishangaa siku ile nilivyomfurahia Jane wakati si kawaida yangu”
“Basi ndio ujue kuna namna hapo”
Ibra akakumbuka kuhusu biashara yake na kumuomba mkewe kuwa wapite kwanza kwenye biashara kabla ya kwenda nyumbani,
“Hata mimi nilikuwa nataka nikwambie hicho kitu, unajua ni muda sana haujafungua biashara? Ndio mwanzo wa kufilisika huu mume wangu bora umekumbuka leo”
Ibra alipeleka gari moja kwa moja hadi kwenye biashara yao kisha wakashuka na kuelekea dukani, ambapo alifungua duka, ila alishangaa kuona kuna mzigo mpya umejaa ndani ya duka lao, Ibra akamtazama mkewe na kukosa jibu kabisa.
Muda kidogo alisogea baba John pale dukani kwa Ibra na kusalimiana nae, Ibra akamwambia baba John
“Za siku nyingi ndugu yangu?”
“Za siku nyingi kivipi tena?”
“Khee unasahau kama hatujaonana kwa siku nyingi sana, nilikuwa na matatizo mwenzio”
Baba John akacheka kisha akamwambia Ibra,
“Yani wewe ndio umesahau au unaogopa nitakuuliza kuwa mzigo unatolea wapi siku hizi nini? Wewe jana si ulikuwa hapa na tukaongea sasa unasemaje za siku nyingi”
Ibra akawa kimya kwa muda kisha akauliza,
“Jana nilikuwa hapa?”
“Sasa unaniuliza nini tena Ibra jamani? Jana si ulikuwa unashusha mzigo wewe huku ukijisifia kuwa biashara ni nzuri sana siku hizi!”
Sophia akaingilia yale mazungumzo,
“Ila jana yote nilikuwa na mume wangu na hatujafika hapa dukani kabisa, sasa ni jana gani unayoiongelea shemeji?”
“Mnajua msinichekeshe jamani, Ibra kama hukuwa hapa jana huu mzigo kashusha nani? Mzimu wako au? Na niliyekuwa nazungumza nae jana ni nani? Wewe si jana umeniambia kuwa nisikueleze tena habari za waganga wewe……..”
Kabla hawajaendelea na yale mazungumzo baba John akaitwa na kuelekea alipoitwa, Ibra na mkewe wakatazamana kwa muda kisha Ibra akamwambia mkewe,
“Ndio haya haya maajabu ya kumuona Jane nyumbani halafu yeye anakataa kuwa hakuj”
“Kweli haya ni maajabu mume wnagu, unajua nakosa jibu kabisa hiyo jana ni jana gani jamani loh mbona maajabu!”
“Maajabu haswaa, na zaidi ni huu mzigo hapa dukani kauleta nani? Yani Baba John ananishangaza sana kusema kuwa mzigo huu nimeushusha mimi, kwanza sina pesa za kushusha mzigo kiasi hiki mie”
Wakajikuta wakijadili bila kupata muafaka wala kupata jibu la aina yoyote lile.
Muda kidogo alifika mteja na kununua bidhaa kwenye duka lao, kisha wakampatia na kuchukua pesa ila wakati wanafungua droo ili kuiweka ile hela wote walishangaa sana na kutazamana kwani walikuwa droo ikiwa imejaa pesa,
“Ibra zimetoka wapi pesa zote hizo?”
“Sijui yani hata mimi mwenyewe nashangaa tu kuwa zimetokea wapi pesa zote hizo”
“Maajabu haya ujue”
“Ni maajabu kweli”
“Au uliacha pesa umesahau mume wangu?”
“Yani niache pesa zote hizo? Sophy uchumi wangu unaujua kabisa, yani nichukue mzigo halafu niwe na pesa zote hizo nitazitoa wapi? Na hata kama isingekuwa mzigo mpya bado siwezi kuwa na pesa nyingi hivyo”
“Basi tuzibebe twende nazo nyumbani”
Wakakubaliana hivyo na kuchukua mfuko na kuziweka zile pesa ambapo walijaza mifuko miwili kisha wakatoka na kufunga duka halafu wakaelekea kwenye gari yao huku wakipanga kuwa wakifika nyumbani waanze kuzihesabu hizo pesa,
“Yani Ibra hii hela imenipa imani sana moyoni dah! Hela nyingi hivi, umasikini kwaheri, sasa tutaanza kufanana na nyumba tunayoishi”
“Sophia unavyofurahia hiyo hela utafikiri unajua ilipotoka”
“Hata sijali ilipotoka yani cha msingi tumeikuta dukani kwetu, hapa nina furaha hatari natamani tufike tu nyumbani tuanze kuhesabu yani haya ni mamilioni mume wangu. Umasikini kwaheri, hizi hela tumezikuta dukani kwetu kwahiyo ni za kwetu. Kama kuna wezi waliiba huko na kuja kuficha dukani kwetu imekula kwao yani kama vipi hata kile kibiashara tutakifunga”
Ibra akawa anacheka tu kwani alishaona kuwa mkewe amepagawa na zile pesa ukizingatia hajawahi kuona pesa nyingi kiasi kile.
Walipofika nyumbani wakashuka na ile mifuko yao na kuingia ndani, kisha kuzimwaga zile pesa na kuanza kuhesabu kabla ya kufanya kitu kingine. Walitumia muda mrefu kidogo katika kuhesabu zile pesa na walipomaliza wakapiga mahesabu tena na kutazamana,
“Kheee Ibra milioni mia uwiiiii jamani umasikini kwaheri yani kwaheri kabisa, hivi zilikaaje kwenye droo pesa zote hivi? Yani tumejipatia pesa kiulaini kabisa, sisi sio majambazi wala sio mafisadi ila tumejipatia pesa kiulaini, umasikini kwaheri jamani”
“Unajua Sophy mimi bado nashangaa kuwa hizi pesa zimetokea wapi?”
“Acha kushangaa bhana, hebu nikumbushe tena kile kibiashara chako kinamtaji wa shilingi ngapi?”
“Kheee leo inaitwa kibiashara jamani, kuna milioni kumi pale”
“Sasa milioni kumi kitu gani katika milioni mia mume wangu? Kwanza wewe zamani si ulikuwa unauza genge wewe na mtaji wako ambao haukufika hata laki! Kwahiyo hata hiyo biashara ya milioni kumi kwako ilikuwa miujiza, na sasa tunamiliki milioni mia waoooo yani furaha yangu ya leo sijui nani ataizima”
“Ila asophy usifurahi sana hadi tujue chanzo cha hii pesa”
“Acha zako bhana, unataka kunigeuka nini? Tena na mimi nataka uninunulie gari yangu nianze kujidai mie yani watanikoma , watajua jina langu la utoto, watajua kabla sijaitwa Sophia nilikuwa naitwa nani. Uwiiiiii kama najiona vile kwenye maisha ya kifahari na kitajiri”
Ibra akamsikitikia mkewe kwani aliona wazi kuwa ameingiliwa na ulimbukeni wa ile pesa kabisa kwani alionekana kusahau yote yaliyomsibu.
“Ninunulie gari kwanza, yani nataka niende nyumbani na gari yangu ili majirani wote wanishangae mimi jinsi ninavyong’aa kila mtu ajue Sophia kaingia. Atakayenisalimia tu, namchapa na elfu kumi dah haya maisha nilikuwa nayatamani sana”
“Sawa mke wangu, basi tukaweke benki hizi pesa”
“Benki? Tuweke benki ili iweje? Hizi tunatumia mume wangu, kuna msemo unasema ukipata tumia ukikosa jutia hakuna caha kwenda kuweka benki wala nini hapa ni kutumia hizi pesa tu mwanzo mwisho halafu sasa tutakuwa hatuendi tena hoteli mchwara tunatakiwa kwenda zile hoteli babkubwa. Watu husema tumia pesa ikuzoee kwahiyo lazima tutumie hii ituzoee bhana”
Ibra hakubishana na mkewe kwahiyo akakubaliana na maamuzi ya mke wake ingawa kwa kiasi fulani hata yeye zile pesa zilimpagawisha kiasi.
Wakakubaliana kuwa zile pesa waziweke chumbani kwao na kuamua kufanya hivyo ambapo zile pesa wakaziweka kwenye kabati la nguo chumbani kwao huku nguo zingine wakizitoa na kuzihamishia sehemu nyingine kisha wakaamua kwenda kula kwanza,
“Sasa mke wangu tupike au?”
“Tupike!! Kwanini tupike kwanza? Leo tunaenda kula hotelini yani ndio furaha yangu halafu kesho utaenda kuninunulia gari”
“Sawa, twende basi ili tuwahi kurudi”
Wakatoka nje na kuingia kwenye gari yao na kuanza safari, njiani wakaona hoteli kubwa sana na wote wawili kuishangaa ile hoteli,
“Kheee imejengwa lini hii?”
“Nadhani itakuwa mpya”
‘Twende tukale hapo basi”
“Hapana Sophy, twende sehemu ambayo tumeizoea tayari”
‘Hivi nilikwambia nini Ibra? Mambo ya kwenda kwenye hoteli uchwara tuache, twende hiyo mpya tujue kuna nini jipya. Kwani unahofu gani wakati pesa tunayo ya kutosha!”
Ibra akakubali kisha wakakunja na kuingia kwenye hiyo hoteli ambapo waliagiza chakula na kuletewa na kuanza kula, walikula huku wakikisifia kile chakula kuwa kizuri sana mwanzo mwisho.
“Itakuwa hapa kuna wapishi mahili sana”
“Na kweli maana si kwa utamu huu wa chakula”
Walipomaliza vyombo vilitolewa na kisha akaja muhudumu kwaajili ya kuchukua pesa ya malipo ya chakula.
Ibra alifungua ile pochi yake ya mkononi aliyobeba ili kutoa pesa ila alishangaa kuona hakuna pesa ya aina yoyote, akamuangalia mke wake na kumuuliza
“Inamaana hatujabeba pesa?”
“Mmmh hatujabeba pesa kivipi?”
“Sioni hela kwenye waleti yangu”
“Tutafanyaje sasa?”
Mara wakamsikia yule muhudumu akiwaambia,
“Kama mmesahau hela msijali kitu, nitawasaidia”
Kwa pamoja walijikuta wakimuangalia kwa makini huyu muhudumu mwenye moyo wa kipekee, gafla walishangaa kuona kuwa yule muhudumu alikuwa ni Neema kwakweli walishtuka sana.
Itaendelea kama kawaida……….!!!!!!!!!
Toa maoni yako mdau.
NYUMBA YA MAAJABU: 36
Mara wakamsikia yule muhudumu akiwaambia,
“Kama mmesahau hela msijali kitu, nitawasaidia”
Kwa pamoja walijikuta wakimuangalia kwa makini huyu muhudumu mwenye moyo wa kipekee, gafla walishangaa kuona kuwa yule muhudumu alikuwa ni Neema kwakweli walishtuka sana, wakajikuta kwa pamoja wakisema
“Neema!!”
“Ndio ni mimi, vipi mmeona mzuka au?”
“Aaah unafanya hapa kazi?”
“Ndio, mimi ni mpishi mkuu hapa”
“Aaah imekuwaje hadi wakakuajiri hapa?”
“Kwani mimi nina kasoro gani ya kufanya nishindwe kuajiriwa?”
Ibra na Sophia wakatazamana tena, kisha Sophia kwa uoga akamwambia Neema,
“Je tunaweza kuondoka?”
“Njia nyeupe kabisa nimewaruhusu”
Wakainuka huku wakiwa wamejawa na uoga uliopitiliza, wakaelekea kwenye gari yao moja kwa moja na kupanda kisha safari ya kurudi ikaanza huku kila mmoja akishindwa kumuongelesha mwenzie chochote.
Walifika nyumbani na kuingia ndani, walifika sebleni na kukaa kisha wakaanza kuulizana
“Hivi imekuwaje tumetoka bila ya pesa?”
“Hata mimi sielewi imekuwaje”
“Hivi pale isingekuwa Yule Neema tungefanyaje?”
“Ndio hapo sasa, yani hadi saizi najishangaa kuwa ilikuwaje hadi kusahau kubeba pesa jamani!”
“Ila ndio tujifunze mume wangu kuwa tunatakiwa kuishi na kila mtu kwa upendo maana bila Neema pale angetusaidia nani jamani dah!”
“Ila dah najikuta nikiwa na maswali mengi bila ya jibu, kwanza ile hoteli imefunguliwa lini? Neema kaanza kazi pale lini? Mambo mengine yanachanganya sana jamani mmh”
“Halafu unajua nini, mi sikuwahi hata kuona kama kuna ujenzi eneo lile jamani, kweli kuna mambo mengine ni ya siri sana”
“Hivi unakumbuka kuwa lile eneo lilikuwa na nini kabla ya ile hoteli?”
“Hata sikumbuki, ila kesho twende tena tukamlipe Neema na kumpa pesa ya asante kwa kutusaidia”
Muda kidogo wakasikia Yule mtoto akilia,
“Mmmh hivi huyu mtoto ana muda wake maalum wa kulia nini”
Kisha Ibra akainuka na kwenda kumchukua Yule mtoto kisha akaenda nae sebleni,
“Eeeh tufanyaje na huyu mtoto?”
“Tumkorogee maziwa tumpe au umesahau kuwa tumekubaliana kutokumnyonyesha tena?”
“Nakumbuka mke wangu, basi nenda jikoni ukamkorogee hayo maziwa tuje tumpe”
Sophia akainuka na kuelekea jikoni kwa lengo la kwenda kumkorogea maziwa Yule mtoto ili anywe.
Sophia akiwa jikoni wakati anataka kubandika maji, gafla alijiona akisukumwa kwa nguvu na kuanguka chini kisha akahisi chuchu zake zikinyonywa tena kwa nguvu tu kwakweli Sophia alitamani kupiga makelele ila alishindwa na kujikuta akigugumia kwa maumivu tu huku akishangaa kuwa ni nani anayemnyonya maziwa yake bila ya kumuona kwahiyo alikuwa akihangaika tu.
Sebleni nako Ibra alishangaa kuona mkewe hatoki jikoni kwenye uandalizi wa hayo maziwa, ila kilichokuwa kikimshangaza ni kuwa kila alipomtazama Yule mtoto alimuona midomo ikicheza kanakwamba alikuwa ananyonya kabisa na kwa wakati huo alitulia tuli ila kwa haraka haraka Ibra alihisi kuwa ndio kawaida ya watoto kwani wote huwa na tabia hiyo ya kujinyonyanyonya hatakama hawanyonyi kwa muda huo. Akaamua kumuita mkewe ili aharakishe hayo maziwa,
“Sophia, vipi wewe hayo maziwa yanachukua masaa jamani!!! Huyu mtoto anajinyonya midomo atajiumiza bure, lete hayo maziwa bhana”
Sophia hakujibu chochote, na kufanya Ibra amuweke Yule mtoto kwenye kochi ili akamuangalie Sophia jikoni ila alipomuweka kwenye kochi tu Yule mtoto na kuinuka akaanza kulia kamavile kaangushwa chini kwahiyo Ibra alikuwa akirudi na kumbembeleza, alijikuta akifanya hivyo kama mara tano akaona ni vyema ambebe aende nae jikoni.
Alivyofika jikoni alishangaa kumuona Sophia chini akigalalagala, akamshtua
“Sophy, Sophy una tatizo gani mke wangu jamani?”
Sophia akashtuka sana na kumuangalia mume wake kwa jicho lililojaa hofu iliyowazi kabisa,
“Niambie mke wangu nini tatizo?”
“Aaah aaah maziwa yangu…..”
Yule mtoto alianza kulia tena kilio cha ajabu kama ameangushwa vile, Ibra akamkabidhi Sophia Yule mtoto,
“Unanipa wa nini jamani?”
‘Mshike bhana, watoto wa hivi wakiwa na njaa ni bora wakahisi jasho la wamama kuliko la sie vidume”
“Tatizo hujui kilichonipata hata usingenipa huyu mtoto nimshike”
“Nenda kakae nae sebleni ili mimi niandae hayo maziwa maana naona umeshindwa wewe”
Sophia hakuweza kuongea akainuka na Yule mtoto hadi sebleni ambako alifika na kumuweka pembeni ya kochi. Gafla, Sophia alishtukia akipuliziwa kama kitu usoni na kuanguka pale kwenye kochi. Ibra alipotoka jikoni alishtuka sana kwani alimuona Yule mtoto akiwa juu ya Sophia huku akinyonya kwakweli kitendo hiki kilimchukiza Ibra na kumshtua huku akiamini wazi kuwa Sophia hawezi kufanya hivyo, ikabidi amshtue Sophia ila Sophia hakushtuka kabisa na kumfanya Ibra aanze kuingiwa na uoga akaamua kwenda jikoni ili achukue maji aje ammwagie mkewe azinduke ila Ibra alipoingia jikoni tu alishangaa akipiga mueleka hadi chini na kupoteza fahamu kabisa.
Ibra alipokuja kuzinduka ilikuwa giza limeshaingia kabisa, akajikongoja na kwenda kuwasha taa huku akijinyoosha nyoosha bila ya kujua kilichotokea, akatoka mule jikoni na kuelekea sebleni ambapo alimkuta mkewe akiwa na hali ya kutokujitambua kabisa huku Yule mtoto akiwa pembeni kwa muda huu, Ibra akakumbuka kuwa mara ya mwisho alimkuta mkewe akimnyonyesha huyo mtoto kwahiyo moja kwa moja akahisi kuwa mkewe nguvu zimemuisha kutokana na kunyonyesha, Ibra akamsogelea mkewe na kujaribu kumuamsha, muda huu Sophia aliamka ila kwa shida sana na sauti yake ilikuwa chini kama asubuhi moja kwa moja Ibra akahisi kuwa mkewe kazidiwa na njaa akawaza pa kupata chakula kwa muda huo, akachukua simu yake na kuangalia muda akaona kuwa ni saa saba usiku.
“Kheee sasa saba? Jamani imekuwaje tena, yani saa saba hii tutapata wapi chakula sasa?”
Ikabidi ajishauri kuwa aende tu jikoni akampikie mke wake, ila alipofika jikoni alikuta chakula kikiwa cha moto kabisa kwenye sufuria kanakwamba kimepikwa muda sio mrefu, kutokana na hali ya mkewe ikamfanya Ibra asijihoji sana na kupakua kile chakula kisha kwenda nacho sebleni na kuanza kumlisha mke wake ambapo alikula hadi pale alipoonekana kurejewa na nguvu zake. Ibra alimpa pole sana mke wake huku akimuonea huruma sana, yani walikuwa wakizungumza muda huo kamavile kumeshakucha tayari.
“Unajua Ibra mimi nashindwa kuelewa mume wangu, imekuwaje huyu mtoto kuninyonya tena?”
“Hata mimi sielewi na ndio nilikuwa nangoja uwe sawa ili nikuulize kuwa huyu mtoto vipi maana nashindwa kumuelewa kabisa”
“Huyu mtoto si wa kawaida mume wangu, sio wakaida kabisa”
“Sasa tutafanyaje?”
“Tukamtupe, mimi siwezi kuendelea hivi, unajua naweza kufa mimi kwasababu ya ujinga wa huyo mtoto! Tumtupe mume wangu”
“Basi, basi ngoja pakuche ndio tukamtupe”
“Sasa pakikucha tutamtupaje jamani si watu watatuona?”
“Kwakweli mimi siafiki kumtupa huyu mtoto usiku huu, tunatakiwa kuwa na huruma ya kibinadamu kiasi. Pakikucha tutapata jibu tu.”
Walijikuta wakiongea usiku wote kwani hakuna aliyetamani hata kulala huku wakiambiana vitu vya kuwashangaza tu.
Kulivyokucha, Sophia alichukua simu yake na kumpigia Siwema kwa lengo la kumuomba ushauri.
“Yani wewe Sophia wa kunisahau mimi wewe? Leo ndio unanikumbuka loh, haya niambie kuna shida gani tena maana hupigi simu bila ya tatizo ila kama ni maswala ya kuwapeleka kwa waganga sipo tayari”
Siwema alikuwa akifunguka tu kwani tayari walishamkera kuhusu Yule babu aliyekufa,
“Tuna tatizo dada, kuna mtoto tumemuokota sasa katushinda kumlea na tumeamua kumtupa tena je unatushauri nini?”
“Kheee Sophia una akili kweli wewe? Yani mumtupe mtoto kweli? Sio jambo jema hata kidogo, mimi nawashauri labda mumpeleke kituo cha kulelea watoto yatima”
“Ndio wapi huko dada?”
“Hebu usinichekeshe Sophia yani hujui vituo vya kulelea watoto yatima wewe? Hebu kwanza ngoja nije huko kwenu”
“Itakuwa vizuri sana dada, asante”
Simu ikakatika kisha Sophia akamueleza Ibra vile alivyoongea na Siwema,
“Kama anakuja itakuwa vizuri sana mke wangu maana kiukweli nimechoka vituko vya huyu mtoto haswaaa kile kitendo cha kumuona akipanda kifuani kwako na kunyonya”
Muda huu wakaenda kuoga na kunywa chai kabisa kisha wakarudi sebleni wakimsubiri Siwema na kuendelea na maongezi yao ya hapa na pale.
Muda kidogo Siwema aliwasili na kuwagongea mlango, walimfungulia na kumkaribisha ndani. Aliingia na kusalimiana nao kisha kukaa kwenye kochi na kumuona Yule mtoto akiwa amelazwa kwenye kochi pia.
“Kwahiyo mtoto mwenyewe ndio huyo?”
“Ndio ni huyo dada”
“Mmemuokota wapi na nyie?”
“Kwnye gari”
“Kheeee msinichekeshe, kwenye gari mmemuokotaje?”
Ikabidi wamueleze ilivyokuwa hadi kumchukua huyo mtoto,
“Kwahiyo inamaana kuna mtu kawawekea huyo mtoto?”
“Ndio”
“Eeeh anaitwa nani?”
“Kwakweli hatujampa hata jina huwa tunamuitaga mtoto tu hivyo hivyo”
“Na je mlivyomuokota mlienda kuripoti polisi?”
“Hapana”
“Ila kwakweli nyie mnamatatizo sana sijui hata akili zenu huwa zinawaza vitu gani, haya sasa mnataka kumtupa tena bila hata ya kufikiria jamani. Huyu mtoto apelekwe kwenye kituo cha kulelea watoto yatima kama mmeshindwa kumlea, kwahiyo mmekaa nae hapa kwa muda gani na alikuwa anakula nini siku zote mlizokaa nae?”
Wakaanza kumueleza jinsi walivyoishi nae na chakula alichokuwa anakula,
“Mungu wangu, hivi nyie akili zenu ni nzima kweli jamani? Kheee mpo kama watu sijui wa dunia ya wapi? Ona sasa hadi mimba imetoka, ulishindwa hata kuomba ushauri jamani? Haya leteni nguo za huyu mtoto haraka tumpeleke huko”
“Hana nguo zozote zaidi ya hizo alizozivaa’
“Kheeee mnazidi kunipa maajabu, kwahiyo siku zote hizi alikuwa akinya na kukojoa mnamvalisha nguo gani? Hamumuogeshi huyo mtoto?”
“Kwakweli dada toka siku tumeingia na huyu mtoto humu ndani hatujawahi kumuogesha, hajawahi kunya wala kukojoa”
Siwema alizidi kushangaa Yule mtoto na kuwashangaa wanaoishi nae pia, hakutaka kupoteza muda akawaomba wambebe ili apelekwe huko kwa watoto yatima.
Wakambeba na kutoka nae nje kisha kuingia kwenye gari na kuanza safari ya kwenda huko kituoni.
Wakati wanatoka Sophia akaamua kumsimulia Siwema kuhusu hoteli waliyoenda jana na jinsi walivyokutana na Neema, Siwema alishangaa tu na kuwauliza mahali ilipo hiyo hoteli .
“Usijali tutakuonyesha ni mpya kabisa hiyo hoteli”
“Yani ndio imefunguliwa huku duh!”
“Kumeendelea huku siku hizi sio kama zamani”
Walipofika kwenye hiyo njia wakapanga kumuonyesha Siwema hiyo hoteli ila walishangaa ambavyo hawakuiona hiyo hoteli wala nini,
“Sophy, ile hoteli si ilikuwa hapo au nimesahau?”
“Mie nakumbuka vizuri ilikuwa hapo, imekuwaje tena jamani?”
Siwema alipoangalia kwa makini eneo lile alishangaa pia na kuwauliza,
“Mbona eneo lenyewe limeandikwa ni eneo la makaburi sasa hiyo hoteli iko wapi?”
Na wao wakaangalia kwa makini sasa wakaona kibao kilichoandikwa kwa herufi kubwa ‘ENEO LA MAKABURI’ wakatazamana na kushangaa, na walipoangalia vizuri wakaona makaburi mengi tu yamejipanga.
Itaendelea kama kawaida………!!!!!!!
Toa maoni yako mdau.
Disqus Comments