Nduguye Obama kuwa mgeni wa Donald Trump kwenye mdahalo
Maafisa wa kampeni wa mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump wamepanga kumwalika kaka wa kambo wa Rais Barack Obama kuhudhuria mdahalo wa mwisho wa urais nchini Marekani.
Maafisa hao wamesema Malik Obama, ambaye alizaliwa Kenya, atakuwa miongozi mwa hadhira itakayofuatilia mdahalo huo wa runinga, Bw Trump alikabiliana na mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton.
Malik, aliambia gazeti la New York Post kwamba ana furaha isiyo na kifani kwamba atahudhuria mdahalo huo.
"Trump anaweza kuirejeshea Marekani fahari yake tena," amesema, kwa mujibu wa shirika la habari la AP.
Wagombea wamekuwa wakitumia wageni kwenye midahalo kama njia ya kuwakabili wapinzani wao.
Bi Clinton amekuwa akiwaalika wakosoaji wakuu wa Bw Trump, bilionea Mark Cuban na afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Hewlett Packard Enterprise Meg Whitman.
Katika mdahalo wa pili, Bw Trump alialika wanawake watatu amabao walimtuhumu rais wa zamani Bill Clinton kwa kuwadhalilisha kingono miaka ya nyuma.
Malik Obama amekuwa akikosoa utawala wa kakake Rais Barack Obama.
Disqus Comments