Wabunge Yanga wairarua simba
WABUNGE wapenzi wa Yanga jana walitoka vifua mbele baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya wenzao wa Simba katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mchezo huo pamoja na ule uliotangulia wa wasanii wa Bongo fleva dhidi ya Bongo movie, ulikuwa maalumu kwa ajili ya kuchangia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Awali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizindua mfumo wa tiketi za elektroniki kuingia Uwanja wa Taifa na kusema kuwa uko vizuri na unatakiwa kuendelea kutumika.
Alisema ameridhishwa na mfumo huo na unatakiwa kutumika katika viwanja vya michezo, hasa huo wa Taifa ili kuziwezesha timu na nchi kupata mapato zaidi.
Majaliwa aliyasema hayo baada ya kutumia mfumo huo wakati akiingia kushuhudia pambano la Wabunge wapenzi wa Yanga na wale wa Simba ambao walitanguliwa na pambano la wasanii wa Bongo movie na wale wa Bongo fleva.
Katika mchezo wa netiboli, timu ya Bunge iliibuka na ushindi wa mabao 15-14 dhidi ya TBC huku Imelda Hango wa Bunge akifunga mabao tisa na Irene Elias wa TBC alifunga mabao 10 peke yake.
Kwa upande wa soka, timu ya Bongo fleva walishinda kwa penalti 5-4 dhidi ya Bongo movie baada ya timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika muda wa kawaida wa dakika 90 wa mchezo.
Wabunge wa Yanga waliandika bao la kuongoza katika dakika ya tatu lililofungwa na Sadifa Hamisi huku Mohamed Mchengerisa alifunga la pili na la tatu katika dakika ya tano na nane. Omary Mgumba aliifungia Simba bao la kwanza. Yanga walifunga bao la nne na tano katika dakika ya 25 na 28 kupitia kwa Mwigulu Nchemba.
Wabunge wa Simba waliandika bao la pili katika dakika ya 39 lililofungwa kwa penalti na Godfrey Mgimwa.
Kikosi cha wabunge wa Simba: William Geleja, Jaku Hashimu, Hamad Masauni, Kaizer Makame, Omari Mgumba, Godfrey Mgimwa, Paschal Haonga, Cosato Chumi, Hamis Kigwangala, Aziz Aboud na Sixtus Mapunda.
Wabunge wa Yanga: Hamidu Bobali, Venance Mwamoto, Gibson Meiseyeki, Mussa Sima, Ahmed Nguali, Anthony Mavunde, Sadifa Hamis, Ali King, Mohamed Mchengerisa, Ridhwan Kikwete na Alex Ghashaza. Pambano hilo liliingiza jumla ya Sh milioni 187.
Disqus Comments