Na Baraka Mbolembole
MECHI Tano za ligi kuu Tanzania Bara zinataraji kuchezwa Jumamosi hii na nyingine tatu zitapigwa siku ya Jumapili.
Kufikia michezo ya raundi ya tano kwa kila timu, hakuna timu yoyote iliyopata ushindi wa asilimia 100 huku timu za JKT Ruvu ya Pwani na Majimaji FC ya Songea zikibaki kuwa timu pekee ambazo hazijaonja ladha ya ushindi msimu huu.
Simba SC v Majimaji FC
Vinara wa ligi hiyo Simba SC wataendelea kubaki jijini Dar es Salaam na safari hii watawavaa ‘waburuza mkia’ Majimaji FC ya Songea katika Uwanja wa Uhuru.
Kally Ongala, kocha kijana ambaye aliisaidia kwa kiasi kikubwa Majimaji kubaki VPL msimu uliopita ametajwa kurejeshwa kufuatia timu hiyo kufikia makubaliano na mdhamini mpya na sasa Kally anataraji kumvaa ‘bosi’ wake wa zamani Mcameroon, Joseph Omog ambaye walishinda pamoja taji la VPL wakiwa wakufunzi wa Azam FC msimu wa 2013/14.
Simba iliifunga Azam FC wikiendi iliyopita na kufungua ‘pengo’ la pointi 3 zaidi ya Yanga SC na Azam FC. Pointi 13 ambazo tayari wamekusanya katika game tano zinawafanya mabingwa hao wa zamani kuwa juu ya msimamo na wataivaa Majimaji ambayo si tu kwamba haijapata ushindi wowote hadi sasa bali hawana pointi hata moja kufuatia kupoteza game zao zote tano.
Majimaji walifungwa 6-1 msimu uliopita katika uwanja wa Taifa siku ambayo, Ibrahim Ajibu alifunga magoli matatu kwa mpigo ‘ Hat-trick’.
Majimaji imepoteza michezo yote mitano msimu huu huku ikiwa imeruhusu magoli 11 na kufunga magoli mawili tu inakutana na Simba iliyofunga magoli nane huku magoli 7 yakifungwa na raia wa Burundi, Laudit Mavugo aliyefunga mara tatu, Ajib na kiungo-mshambulizi, Shiza Kichuya waliofunga magoli mawili mawili kila mmoja.
NDANDA FC v AZAM FC
Baada ya kupata ushindi wa kwanza wikiendi iliyopita, timu ya Ndanda FC watarejea katika uwanja wao wa Nangwanda, Mtwara. Safari hii watawavaa ‘majeruhi’ Azam FC ambao walichapwa 1-0 na Simba wiki iliyopita.
Ndanda ilishinda 2-1 ugenini dhidi ya Majimaji bado inasumbuliwa na safu yao ya ulinzi ambayo imesharuhusu magoli sita katika michezo mitano iliyopita. Wamefanikiwa kufunga magoli manne jambo ambalo linaashiriia wana uwezo wa kufunga.
Azam wakiwa nafasi ya tatu na alama zao kumi watamtegemea mshambuliaji na nahodha wao John Bocco ili kupata magoli baada ya kushindwa kufanya hivyo dhidi ya Simba. Bocco amefunga magoli matatu kati ya 7 ya timu yake msimu huu ataongoza mashambulizi kwa mara nyingine.
Mtibwa Sugar FC v Mbao FC
Wikiendi iliyopita kulikuwa na ‘mshangao mkubwa’ katika VPL ambapo ilishuhudiwa Mbao FC ya Mwanza ikipata ushindi wake wa kwanza katika historia ya ligi kuu Bara. Timu hiyo iliichapa Ruvu Shooting ya Pwani magoli 4-1 katika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.
Jumamosi hii watakuwa Manungu Complex, Turiani, Morogoro kuwavaa Mtibwa Sugar. Mabingwa hao mara mbili wa zamani ( 1999 na 2000) wapo nafasi ya tano katika msimamo wakiwa na alama 9 waliichapa Kagera Sugar wiki iliyopita katika uwanja huo wameanza kurejea katika kasi yao ya kawaida kufuatia kuwapoteza wachezaji wengi msimu huu.
TANZANIA PRISONS v MWADUI FC
Mechi nyingine kali siku ya Jumamosi hii ni ile itakayowakutanisha Tanzania Prisons ya Mbeya na Mwadui FC ya Shinyanga katika Uwanja wa Sokoine.
Prisons imeshinda game mbili na ilipata sare ya pili Jumamosi iliyopita walipopambana na ndugu zao Mbeya City FC katika ‘ Mbeya-Pacha.’ Kikosi hicho cha Meja Mstaafu, Mingange kimeshapoteza mchezo mmoja katika uwanja wa nyumbani msimu huu kinakabiliwa na tatizo la umaliziaji.
Katika michezo yao mitano wamefanikiwa kufunga magoli matatu tu na kuruhusu mawili, wataikabili Mwadui iliyo nafasi ya tatu kutoka mkiani.
Kikosi cha kocha Jamhuri Kihwelo kimeshinda mechi moja na kupata sare moja huku kikichapwa mara tatu katika michezo mitano iliyopita, nao wanasumbuliwa na tatizo la ufungaji kwa kuwa hadi sasa wamefunga magoli matatu tu.
Safu ya ulinzi ya Mwadui pia imekuwa na tatizo la kuruhusu magoli mara kwa mara ndiyo maana wameshakubali magoli sita katika nyavu zao. Ni mechi ambayo kwa namna yoyote, Julio hapaswi kuangusha pointi tatu na kuruhusu hilo ni sawa na kufungua presha ya kutimuliwa katika kibarua chake.
JKT RUVU v MBEYA CITY FC
JKT RUVU v MBEYA CITY FC
JKT Ruvu imefanikiwa kupata sare mbili na kupoteza michezo miwili katika game zao nne za msimu huu. Jumamosi hii watawavaa Mbeya City FC katika game nyingine inayotaraji kuwa na upinzani mkali.
City chini ya mkufunzi, Mmalawi, Kinah Phiri imeanza vyema msimu huu kwa maana ushindi mara mbili na sare mbili zimewafanya kufikisha alama nane ambazo zimewaweka katika nafasi ya 6. Timu hiyo ya ‘Kizazi Kipya’ itaendelea kumtegemea mshambuliaji wake kijana, Rafael Daud ambaye ameshafunga magoli matatu kati ya 6 ya timu yake.
JKT Ruvu inasotea ushindi wa kwanza msimu huu inataraji kuongozwa na washambuliaji, Samwel Kamutu na Atupele Green.
SEPTEMBA 25
Stand United FC v Yanga SC
Mabingwa watetezi Yanga SC watabaki katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kuwavaa Stand United siku ya Jumapili. Babda ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Mwadui FC wikendi iliyopita, kikosi cha Mholland, Hans Van der Pluijm kitawavaa Stand.
Ni mechi itakayowakutanisha timu ambazo hazijapoteza mchezo hadi sasa. Licha ya matatizo kadhaa katika uongozi kikosi cha Mfaransa, Patrick Liewig kimeendelea kuwa imara ndani ya uwanja. Stand imeshinda mechi mbili na kupata sare 3, hivyo kukusanya alama 9 ambazo zimewapandisha hadi katika nafasi ya nne.
Mshambuliaji mzoefu, Adam Kingwande ameshaifungia timu hiyo magoli mawili kati ya matano waliyokwisha funga. Yanga ndio timu pekee isiyoruhusu goli hadi sasa, inashika nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na alama kumi.
Mechi nyingine siku ya Jumapili hii ni zile za Shooting v Toto Africans ya Mwanza na mechi ya mwisho itakuwa kati ya African Lyon v Kagera Sugar