-->

MAGUFULI ATAKA DIPLOMASIA IKUZE VIWANDA

RAIS John Magufuli, ametaka utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utiliwe mkazo katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda. Aliyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam juzi jioni alipokutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani. Mkutano huo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ulihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Rais Magufuli aliyehutubia na kuongoza majadiliano juu ya masuala mbalimbali ya shughuli za mabalozi, alisema Tanzania imeweka dhamira ya kuikuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia 7.3 hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2021 na kuzalisha ajira kwa asilimia 40. “Sasa nimeona niwaite waheshimiwa Mabalozi ili tuelewane, mjue mwelekeo tunaoutaka na mjue ni namna gani mtakavyoshiriki kuhamasisha uwekezaji wa viwanda. “Nataka badala ya kubaki mmejifungia ofisini, mtoke mwende mkawatafute wawekezaji waje wawekeze katika viwanda ili nchi yetu inufaike kwa watu wetu kupata ajira, Serikali kukusanya kodi na tuinue maendeleo yetu,” alisema Rais Magufuli. Maeneo mengine ambayo Rais alitaka Mabalozi wayafanyie kazi ni kutangaza na kuwavutia watalii kuja nchini, kufanyia kazi fursa zote zenye manufaa kwa Tanzania katika nchi wanakowakilisha, kulinda mali za nchi zilizopo katika nchi hizo na kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya biashara na uwekezaji inayofanywa kati ya Tanzania na nchi wanakowakilisha. Aliwataka Mabalozi wote kufanya kazi kwa juhudi, kuondoa kasoro za utendaji kazi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa katika ofisi zao na kubana matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima. Rais pia aliitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujipanga na kudhibiti mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha za umma ambazo zimekuwa zikitumika katika safari za nje ya nchi na matumizi mengine yasiyo ya lazima. Aliwaagiza kuhakikisha watumishi wote ambao wapo katika ofisi za ubalozi kwenye nchi mbalimbali bila sababu za msingi wanarejeshwa nchini ili kupunguza mzigo wa gharama kwa Serikali. “Kuna wafanyakazi wapo kwenye Balozi zetu wakati hata sifa za kuwa katika nafasi wanazoshikilia hawana, ilifika mahali mtu akiharibu hapa nyumbani anapangiwa ubalozini. “Wakati mwingine unakuta Ubalozi wa Tanzania kwenye nchi fulani una idadi kubwa ya wafanyakazi kuliko mahitaji ya ubalozi huo, haiwezekani,” alisisitiza. Hata hivyo aliwapongeza Mabalozi wote wa Tanzania kwa kazi wanazozifanya kwenye nchi wanazowakilisha na aliwahakikishia kuwa Serikali ina matumaini nao na inawategemea kuwa wataendelea kuiwakilisha na kuitangaza vizuri Tanzania. Mkutano huo pia ulihuduriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa taasisi mbalimbali na Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Nemo enim ipsam voluptatem quia voluptas sit aspernatur aut odit aut fugit, sed quia consequuntur magni dolores eos qui ratione voluptatem sequi nesciunt.

Disqus Comments